Viongozi wa mrengo wa Azimio walikemea hatua ya kukamatwa kwa aliyekuwa gavana wa Kakamega Wyclife Oparanya wakidai kuwa ni lengo la kutaka kumhangaisha kabla ya ziara ya rais Ruto katika eneo la Magharibi.
Oparanya na mkewe walikamatwa kwa madai ya ubadirifu wa takriban shilingi bilioni 1.3 kwa makosa ya uhalifu wa kiuchumi ambayo wanadaiwa kuyatekeleza wakati alipokuwa mamlakani.
Oparanya hata hivyo alijitetea katika mazungumzo yake na waandishi wa habari kuwa hakuna uchunguzi wala madai yoyote ya ufisadi aliyohusishwa na Tume hiyo kuazia alipochukua hata hatamu ya kwanza uongozini kama waziri wa Mipango hadi alipokuwa Gavana wa Kakamega.
“Nimehudumikia serikali ya kaunti kwa miaka 10 hakuna afisa wa EACC aliwahi kufika katika afisi yangu hata siku moja, nimekuwa nje ya Gavana kwa mwaka mmoja sasa hakuna aliyenikabili kwa uchunguzi wowote, nilikuwa Waziri wa mipango hakuna aliyefika katika afisi yangu kwa uchunguzi. Nashangaa kwanini baada ya kustaafu mtu aje kuniuliza kuhusu mwaka 2013,2014.” Alisema.
EACC kwa upande wake imekaza kamba kuwa uchunguzi huu ulikuwa ukiendelea kwa muda katika kaunti kadhaa ambazo ziko kwenye kurunzi yao kufuatia tuhuma za ufisadi.