Mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa wa Buxton Point uliogharimu shilingi bilioni 6 umekamilika.
Mradi huo ulitekelezwa na Kampuni ya Gulf Cap Real Estates na sasa nyumba hizo zinatarajiwa kukabidhiwa wamiliki wake Jumamosi hii.
Mnamo siku ya Jumamosi Septemba 16 milango ya nyumba za Buxton point itafunguliwa rasmi, wamiliki wakikabidhiwa rasmi nyumba zao baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika.
Akizungumza na vyombo vya habari Alhamisi, Septemba 14, Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Chris Ochieng amesema mipango imekamilika kukabidhiwa nyumba hizo wanunuzi, akisema kuwa kampuni ya Gulf Cap Real Estates ndiyo ya kwanza kufanikisha mradi wa serikali ya ujenzi wa nyumba za gharama ya chini kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Mombasa.
“Tumeweza kufanikisha ujenzi huu wa buxton awamu ya kwanza ambayo ni vijumba 584 na hivi karibuni tunapania kuzindua rasmi awamu ya pili ya mradi huo ambayo ni takriban nyumba 1400 ili wanunuzi waanze kuishi,na tunafurahi kuwakaribisha walionunua nyumba zetu na tunataka wanapate kuishi maisha mazuri.”Alisema Chris Ochieng.
Ochieng aliongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ambao umejumuisha nyumba 584 umekamilika huku wateja wakusubiri kukadhibiwa nyumba zao rasmi tarehe 16 Jumamosi ya wiki hii.
Kadhalika alisema kwamba wamiliki wa nyumba hizo watakuwa na meneja ambaye jukumu lake kuu litakuwa la kuwasijali katika mipango kadha inayopatikana eneo hilo.
“Misingi ya kisasa tuliyoweka imekamilika, sio tu kukabidhi nyumba hizi kwa wenyewe bali kuwawezesha kuishi maisha ambayo wamekuwa wakiyatarajia ndio maana tunahimiza wanunuzi kujitokeza na kujisajili siku ya Jumamosi.”Aliongeza Ochieng.
Ochieng alibainisha kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba zaidi ya 1400 imeng’oa nanga huku akiwasihi waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza kutuma maombi kwenye awamu ya pili.
“Tunahimiza wale ambao hawakupata nafasi kumiliku nyumba awamu ya kwanza kujisajili na awamu ya pili ya mradi huu.Ujenzi huu unaenda kwa kasi na utakamilika muda usiokuwa mrefu.Tunataka kuwa kielelezo cha ujenzi wa nyumba za bei nafuu Afrika Mashariki.” Alikariri
BY DAVID OTIENO