HabariKimataifaNewsWorld

Watu 13 Wafariki Katika Moto Ndani ya Klabu Moja Uhispania

Takriban watu 13 wamefariki katika mkasa mbaya wa moto ulioteketeza klabu ya usiku ya Burudani nchini Uhispania, huku kukiwa na hofu kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka zaidi huku huduma za dharura zikitekelezwa kutafuta wahasiriwa zaidi.

Chanzo cha moto huo uliozuka mapema Jumapili Oktoba mosi katika ukumbi wa Teatre kusini mashariki mwa mji wa Murcia bado hakijajulikana.

Katika kisa hicho watu wanne walijeruhiwa miongoni mwao wakiwa wanawake wawili, wenye umri wa miaka 22 na 25, na wanaume wawili, wenye umri wa miaka 41 na 45, ambao wote walipelekwa hospitalini kutokana na kuvuta moshi mwilini, tovuti ya huduma za dharura ya Murcia ilibaini.

Manusura waliokusanyika nje ya klabu hio usiku wa tukio walielezea tukio hilo kwa waandishi wa habari wakati wakipokea huduma za dharura.

“Nadhani tuliondoka (klabu) sekunde 30 – dakika 1 kabla ya kengele kulia na taa zote zilizima mayowe yakisema kulikuwa na moto. Nilikuwa mahali ambapo ningeweza kutoka, lakini wanafamilia watano na marafiki wawili hawapo,” alisema mmoja.

“Hatujui chochote, tunasubiri habari ili kuona kama baadhi ya wanafamilia wetu wametoka hai,” alisema mtu mwingine katika eneo la tukio.

Wakati wa tukio hilo, huduma za dharura zilitumwa, huku wazima moto wa eneo hilo wakiita msaada wa helikopta kukabiliana na moto huo.

“Mkurugenzi Mkuu wa Usalama na Dharura, Ricardo Villalba, yuko kwenye tovuti akiratibu na Halmashauri ya Jiji la Murcia njia muhimu za kudhibiti janga hili,” idara ya huduma za dharura ilisema.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alituma salamu za rambirambi.

“Upendo wangu na mshikamano kwa wahasiriwa na familia za moto mbaya uliotokea asubuhi ya leo katika kilabu cha usiku huko Murcia. Nimemjulisha rais wa eneo la Murcia msaada wetu na ushirikiano wetu,” Sanchez alichapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, uliojulikana kama Twitter.

Mkasa huo mjini Murcia Umeingia katika historia ya ajali mbaya kuwahi kutokea katika klabu za usiku nchini Uhispania kwa kipindi cha miaka 33 ambapo mnamo mwaka 1990 Moto katika klabu moja ya usiku kaskazini mashariki mwa Zaragoza ulisababisha vifo vya watu 43. Mnamo Desemba 1983 watu 81 waliuawa katika moto wa klabu ya usiku huko Madrid, na kupelekea maafa.

Hata hiyo Siku tatu za maombolezo zimetangazwa katika jiji la Murcia kwa ajili ya “wale waliofariki katika moto uliotokea kwenye klabu hio ya Teatre de Atalayas”, meya wa Murcia José Ballesta alisema kwenye X.

Eneo la habari kwa jamaa za wahasiriwa lilianzishwa katika eneo la karibu la Palacio de los Deportes, ambapo timu ya wanasaikolojia itapewa jukumu la kutoa msaada.

BY EDITORIAL DESK