Mhubiri Ezekiel Odero alibaini kuwa yu tayari kufika mbele ya kamati ya Bunge la Seneti kutoa maelezo kuhusu kanisa lake na madai ya kuhusishwa na mauaji ya halaiki ya Shakahola.
Odero ambaye alijitenga mbali na maafa ya Shakahola, akiri hana jambo la kuficha na ataweka bayana kila kitu mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Tana River Danson Buya Mungatana.
Odero maarufu pasta Ezekiel, aliagizwa kufika mbele ya kamati hiyo ya seneti inayochunguza mauaji hayo ya halaiki na anatarajiwa kuhojiwa ili kubaini ushirika wake na kanisa la mchungaji tata Paul Mackenzi, GNI.
Mawakili wake Danstan Omari na Cliff Ombeta waliokuwa wakiandamana naye walieleza kuwa watawasilisha ushahidi kwa kamati hiyo ikiwemo video katika juhudi zao za kumtetea mteja wao.
“ Wanataka Odero afike mbele ya kamati ya seneti atoe maelezo kuhusiana na mambo yafuatayo. Kwanza ni kuhusu uhusiano wake na mhubiri Paul Mackenzie. Pili ni kuhusiana na stesheni yake ya televisheni ambapo msimamo wa Ezekiel umekuwa kwamba alitaka kununua stesheni ya televisheni kutoka kwa Mackenzie na akatoa deposit ya shilingi laki 5 lakini biashara hiyo haikufanikishwa hivyo basi akanunua stesheni nyengine. Leo tutatoa ushahidi kuonyesha fedha zinazopokelewana Ezekiel hutoka kwa sadaka za waumini na njia nyengine.”
Tayari Mhubiri tata Paul Mackenzie anayetuhumiwa kwa mauaji ya halaiki katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi kupitia Wakili wake Wycliff Makasembo amekataa kufika mbele ya kamati ya seneti inayochunguza mauaji hayo hadi pale kesi yake itakapokamilika.