HabariNews

Barua ya Mackenzie! DCI Yamchunguza Kuhusu kushawishi wenziwe Kizuizini

Idara ya upelelezi DCI inachunguza barua ya mhubiri Tata Paul Mackenzie iliyowaagiza wafuasi wake ambao wamezuiliwa kufunga hadi kufa.

Inaaminika kuwa barua hiyo iliandikwa mnamo Julai 2 ambayo ilinaswa na maafisa wa gereza la Shimo la Tewa wakati wa ukaguzi wa kawaida wa usalama gerezani.

Kulingana na barua hiyo iliwataka washukiwa wanaozuiliwa kuendelea kufunga hadi kifo.

Inspekta mkuu wa Polisi wa eneo hilo Raphael Wanjohi ambaye pia ni mpelelezi mkuu wa mauaji ya Shakahola alisema kuwa barua hiyo ilifichua imani potovu inayoendelezwa kuzuizini.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maafisa wa polisi barua hiyo inaaminika kuandikwa na mshirika wa karibu wa Mackenzie kisha kuidhinishwa na Mackenzie mwenyewe.

Haya yanajiri huku Mahakama ya Shanzu ikiamuru kuzuiliwa kwa Makenzie na washirika wake 27 kwa siku saba zaidi.

Wakati uo huo Mhubiri huyo tata amekataa kufika mbele ya Kamati ya Seneti inayochunguza mauaji ya Shakahola anayohusishwa nayo.

Kupitia Wakili wake Wycliffe Makasembo, Mackenzie aliiambia mahakama ya Shanzu kuwa hayuko tayari kwenda mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Tana River Danson Buya Mungatana hadi kesi yake iliyoko mahakamani itakapokamilika.

Hata hivyo hakimu wa mahakama hiyo hakuzungumzia swala hilo wakati akitoa maamuzi ya ombi la kuendelea kumzuilia mhubiri huyo na washirika wenza 27.

BY MJOMBA RASHID