Kushirikisha umma, utawala bora, uadilifu, uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu imetajwa kuwa kanuni kuu za uongozi bora.
Haya ni kwa mujibu wa katibu katika idara ya ulinzi na maswala ya jamii Joseph Motari aliyesisitiza haja ya uwazi na kushirikishwa umaa ili kutoa maoni na mapendekezo wanayotaka yajumuishwe kwenye bajeti ya mwaka 2024/25.
Akizungumza wakati wa kongamano la uhusishwaji wa maoni ya umma kuhusu makadirio ya bajeti hio mjini Mombasa Motari alielezea matumaini ya kongamano hilo kukuza ushirikishi wa mchakato wa bajeti ya mwaka ujao na kuwezesha kukabiliana na changamoto mbali mbali ikizingatiwa kwa muda sasa wananchi hajakuwa wakihusishwa kwenye makadirio ya bajeti.
“Tumekuja kuanzia mashinani kuskiza maoni ili wao wenyewe wachangia kwenye miradi ambayo wanataka iwekwe kwenye bajeti ya mwaka ujao ,hii kuchukua maoni kwa wananchi ilifanywa mwisho mwaka wa 2011/2012.” Alisema Matori.
Akigusia swala la mpango wa inua jamii Motari alisema kuwa serikali inafanya juhudi zote kuhakikisha walengwa wananufaika badala ya kuishia kwenye mifuko ya watu akiongeza kuwa pesa za mwezi wa Oktoba ziko tayari.
“Mambo ya ufisadi hatutaruhusu nachukua fursa hii kama kiongozi wa wizara hiyo kuambia wazee walemavu na wote wanaopokea pesa hizo kwamba ziko tayari za mwezi wa kumi kwa sasa tumeongeza machifu ili kutupa ujumbe iwapo kuna mabadiliko yoyote.”Alisema Matori.
Kulingana na Zuber Nuru Hussein mmoja wa baraza la wazee kaunti ya Mombasa, hatua ya ushirikishwaji wa umma katika maswala ya makadirio ya bajeti ya mwaka ujao itapelekea kujumuishwa kwa maoni yao kwa maendeleo ya taifa zima.
“Kwa mara ya kwanza serikali imetoa nafasi kwa wananchi wa Mombasa kuhusika kutoa maoni na matarajio ya makadirio ya bajeti ya mwaka ujao, kwanza utasaidia kutenga fedha kwa yale ambayo wananchi wanayataka.” Alisema Nuru