Viongozi wa Kenya Kwanza wameendelea kutetea ziara zake Rais William Ruto za nje ya nchi wakizitaja zenye manufaa kwa Taifa
Akizungumza na waandishi wa habari katika kiako chake cha kwanza tangu kuteuliwa kwake, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura alibaini kuwa safari 39 ambazo Rais William Ruto alifanya chini ya mwaka wake mmoja uongozini zimewezesha serikali kusaini makubaliano ya zaidi ya Trilioni 2 na mataifa ya nje.
Katika kile kinachoonekana kuwakosa wale wanaopinga safari za rais Ruto Mwaura amesema kuwa ziara hizo zimezalisha makubaliano yanayoafiki viwango hivyo vya pesa.
Mwaura aliongeza kuwa mazungumzo yake Rais Ruto na Waziri Mkuu wa Amerika Rishi Sunak yalizalisha takribani bilioni 900 ambazo zitatumika kwenye mradi wa mji wa reli ya kisasa Nairobi itakayoleta mapinduzi kwenye mfumo wa usafiri jijini humo.
“Tukiwa na uwekezaji wa shilingi bilioni 900 nchini, itakuwa hatua mwafaka ya ukuaji maradufu. Mradi mkubwa wa reli ya kisasa Jijini Nairobi ambao utaleta mapinduzi makubwa katika mfumo wa usafiri jijini,” alisema Mwaura.
Mwaura aidha alidokeza kuwa mazungumzo baina ya Rais na Taifa la Senegal yatafungulia zaidi soko la bidhaa za taifa la Kenya.
Kulingana na Msemaji huyo wa Serikali rais tayari aliweka saini Mikataba ya makubaliano katika biashara, Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Kawi, uchukuzi, elimu. leba na usalama na kufungua nchi kwa nafasi zaidi za kibiashara.
“Ikiwa tuna Wakenya 350,000 wanaosafiri kwenda ugahibuni, hebu fikiria ni kiwango gani cha fedha kinachotumwa nyumbani, ikiwa kwa sasa tunapata shilingi bilioni 750 kutoka kwa Wakenya walioko nje,” alisema.
Wakati uo huo Msemaji huyo wa Serikali alibaini kwamba kama si serikali kudhibiti mafuta ya Petroli, bei ya mafuta hayo ingeongezeka maradufu.
Alisema serikali ililazimika kuingilia kati kutumia pesa za umma kudhibiti mfumo wa bei ya mafuta akikanusha kuwa hatua hiyo sio ruzuku kama ilivyosemekana.