Shughuli za usafiri zimetatizika katika barabara kuu ya Mombasa Malindi kufuatia daraja kwenye mto Mbogolo kukatika kufuatia mvua kubwa kunyesha usiku wa kuamkia Novemba 25.
Mvua hiyo imekwamisha wasafiri wanaotumia magari na pikipiki eneo hilo, huku wanaotembea kwa miguu wakiruhusiwa kutumia daraja jipya ambalo halijakamilika.
Caleb Mulira mhandisi anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo alisema kuwa juhudi za kurejesha hali ya kawaida kwenye daraja hilo zinaendelea huku akieleza kuwa wanatarajia kwamba tatizo hilo litapata suluhu jioni yake.
” Haya maji yanapita na juu ya Daraja la zamani na yanapita kwa Kasi sana ikakata pande mbili zote za Daraja lile la zamani. Sasa Daraja Hilo linaelea maji yanaanza kuenda chini lakini hio barabara haipitiki” alisema
Kwa upande wao madereva wa magari ya uchukuzi wa umma walilalamikia kuathirika kwa biashara yao wakisema kuwa wanakadiria hasara kubwa kwa kukosa kufanya kazi pamoja na kulazimika kupeleka magari yao gereji ili kuwekwa vipuri.
” Leo tunapata hasara sababu Mafuta yamepanda na abiria wamelipa pesa na wanakuja hapa kuregeshewa pesa zao, Sasa tumeenda hasara kuwabeba
” tunachokiomba ni serikali itusabidie, ng’ombe zimeenda na maji, Daraja limeenda na maji” Walilalama madereva
Ikumbukwe watumizi wa barabara eneo la Mtondia wamelazimika kutumia barabara ndefu ya Bofa Kwa Ngala, ili kukwepa maji yaliyoziba barabara hiyo kuu kutokana na kufurika kwa mto Mtondia.