HabariNewsSiasa

Imefika Kooni! Jaji Mkuu Koome akomaa ajibu mapigo! Aongoza Mahakama kukashifu kauli ya Rais

Hatimaye Jaji Mkuu nchini Martha Koome amejitokeza kuzungumzia shutma zilizoelekezewa idara ya mahakama na rais Ruto aliyeidai idara hiyo inahusika na ufisadi kukwamisha miradi muhimu ya serikali.

Jaji Mkuu ameongoza maafisa wa idara hiyo kukashifu na kukosoa matamshi ya rais Ruto kuhusiana na utendakazi wa idara hiyo.

Koome amewataka maofisa wa mahakama kuendelea na kazi pasipo kutishwa na mtu yeyote wala upendeleo, huku akibaini kuwa afisi yake itaendelea kulinda kanuni ya kikatiba kutekeleza majukumu yake bila maelekezo kutoka kwa idara nyingine yoyote.

Katika taarifa yake ndani kwa majaji na maafisa wengine wa idara hiyo siku ya Jumatano, Jaji Mkuu alikashifu matamshi ya rais yaliyolenga kesi ambayo ingali mahakamani, matamshi ambayo amesema yanalenga kuhujumu na kutishia majaji kutoa uamuzi kwa namna fulani.

“Ofisi yangu itaendelea kulinda kanuni ya kikatiba inayohakikisha utekelezaji wa majukumu ya mahakama kutekelezwa pasi udhibiti au maelekezo kutoka kwa mtu au mamlaka yoyote. Nawahimiza muendelee na majukumu yenu ya korti bila woga wala upendeleo na kwa kuzingatia kiapo cha mahakama,” alisema.

Koome aidha alisisitiza njia sahihi ya kupinga uamuzi wa korti iwapo mtu yeyote hakuridhika na uamuzi ni kupitia kukata rufaa au kupitia mahakama ya upeo.

“Kuwashambulia majaji na maafisa wa mahakama waliotoa uamuzi hadharani kunadhoofisha maadili ya utaratibu wetu wa kikatiba.” Alisema Jaji Mkuu.

Koome ametaka madai yoyote ya utovu wa nidhamu au vitendo vya ufisadi vya majaji au maafisa wowote wa mahakama kuelekezwa kwa tume ya Huduma za Mahakama JSC kwa hatua mwafaka za haraka kuchukuliwa.

Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Jumanne rais William Ruto akiwa huko kaunti ya Nyandarua alitishia kukiuka uamuzi wa mahakama akitaja majaji kuwa mafisadi.

Taarifa ya Jaji Mkuu sasa inaonekana kujibu shutma hizo za rais akisema kuwa maafisa wa serikali wanapotishia kukaidi amri za mahakama utawala wa sheria unahatarishwa na kuweka taifa katika mazingira ya machafuko.

Hata hivyo jaji Mkuu huyo amedokeza kuwa atatafuta kikao na rais na Bunge ili kutatua utata na tofauti zinaoendelea kurindima.

BY MJOMBA RASHID