Shirika la Fedha Duniani, IMF limeidhinisha mkopo mpya wa zaidi ya dola milioni 941 kwa taifa la Kenya ili kusaidia kufadhili taifa hili kukabiliana na changamoto mbalimbali za kifedha.
Kwa mujibu wa IMF, bodi yake kuu imeidhinisha mkopo huo wa Dolla milioni 941.2 ambapo tayari Dolla milioni 624.5 zimeshatumwa.
Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Washington limesema lilitabiri ukuaji wa uchumi wa Kenya kwa karibu asilimia tano mwaka huu, kutoka wastani wa asilimia 5.1 mwaka wa 2023.
Kenya inakabiliwa na changamoto kadhaa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na madeni, gharama ya juu ya maisha na kushuka kwa thamani ya shilingi.
Serikali ya Kenya imetetea hatua ya kuendelea kukopa ikisema kuwa ni njia moja ya kuimarisha mifumo ya sera pamoja na kuendeleza miradi ya serikali.
Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Wizara ya Fedha mwezi huu, deni la umma la Kenya limefikia shilingi trilioni 10.585 ambazo ni sawia na (dola bilioni 65.5 za kimarekani).