Kamati ya kitaifa ya nyumba imetoa wito kwa shirika la kitaifa la nyumba
kutowafurusha wakazi kikatili wakati wa kuchukua ardhi za serikali.
Kufuatia ubomozi wa nyumba katika eneo bunge la Changamwe juma
lililopita, sasa kamati ya kitaifa ya nyumba imetoa wito kwa shirika la
kitaifa la nyumba kutumia njia za kiutu wakati wa kuwahamisha wakazi.
Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo na aliyepia mbunge wa Emurua
Dikirr Johana Ng’eno licha ya nyumba zilizobomolewa kuwa za serikali
njia iliyotumika kuwahamisha wakazi wa eneo hilo haikuwa sawa akieleza
kuwa kungefaa kuwa na mwafaka baina ya pande zote mbili wa jinsi
uhamisho huo utakavyofanyika.
“Halafu shirika la kitaifa la nyumba kwasababu hizo nyumba ni zao
walikuja wakajenga nyumba nyingine za ghorofa kando ya zile za zamani
kwasababu walikuwa na shamba kubwa na walikuwa wanataka kujenga nyumba
nyingi kwa hivyo wakajenga nyumba nyingine na wakahamisha baadhi ya
wakazi waliokuwa wakiishi kwenye nyumba za kawaida. Na kwasababu
tulikuwa huko na mbunge wa eneo hilo mheshimiwa Mwinyi, tukawaeleza
wananchi kuwa wakati serikali ikitaka kuwahamisha kwenda kwenye nyumba
mpya tafadhali lazima mjiandikishe na mkubaliane jinsi mtakavyohamishwa
kwenye hizo nyumba.” alisema Ng’eno.
Aidha amesema kamati hiyo itaendelea kusistiza kuwa sheria inafaa
kufuatwa katika kila hatua ya uhamisho wa wananchi kutoka kwa makazi yao
ili kuepuka migogoro.
Hata hivyo ameongeza kuwa kamati ya kitaifa ya nyumba itazuru eneo hilo
hivi karibuni ili kufahamu kwa kina utata uliopo baina ya wananchi wa
eneo bunge la Changamwe na shirika la kitaifa la nyumba.
“Na tuliambia serikali kwamba hizi nyumba zisivunjwe kabla wale watu
ambao walikuwa wanaishi kwenye nyumba hizi wamewekwa sawa kwasababu sisi
kama Wakenya hatutaruhusu yale mambo yanayofanyika hapa Kenya saa
nyingine.
Watu wanabomolewa nyumba wanafanyiwa mambo mengi ndiposa tukasema hao
watu lazima wawekwe sawa na huo ndio msimamo wetu na hata leo kuna wale
watu walileta ombi bunge na sisi tulikuwa tumalize hii kazi mapema ndio
tuende tukasikilize hayo maombi ya kupinga ya hawa watu wa Changamwe
kwamba hawa watu wanafaa kupelekwa wapi baada ya kuondolewa hapa.
Kwa hivyo mambo ya kuvunja nyumba yangekuja mwisho baada ya kila mtu
amehamishiwa kwenye nyumba mpya kwa hivyo sielewi. Lakini kwa upande
wangu na kamati yetu tunataka kila mkenya apewe heshima wala sio vile
tunavyoona wakati mwengine. Na tungependa pia kutoa ushauri kwamba
wakati wa kuwahamisha wakazi lazima wahamishwe kwa njia ya heshima na
sawa.” alisema Ng’eno.
Hayo yamejiri wakati wa kikao cha wananchi kutoa maoni yao kuhusu mpango
wa serikali wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu mjini Kilifi.
BY ERICKSON KADZEHA.