Mchakato wa kamati ya kitaifa ya nyumba kuzuru maeneo mbali mbali nchini kukusaya maoni ya wakazi kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba za bei rahisi ukiendelea wakazi sasa wanatilia shaka mchakato huo kufuatia agizo lililotolewa na mahakama kuhusu mradi huo.
Hofu imeibuliwa na wakazi mjini Kilifi wakati wa kamati ya kitaifa ya nyumba ilipozuru eneo hili kukusanya maoni ya wakazi kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, kufuatia kile kinachodaiwa kuwa ukiukaji wa agizo la mahakama.
Kulingana na Triza Nafula Bwire ofisa wa shirika la Sema Nami Mama, Wakenya wanashangaa hatua ya kamati hiyo kuendeleza vikao hivyo akiitaka serikali kujitokeza wazi wazi na kufafanua swala hilo ambalo linasalia kuwa kizungumkuti kwa wakenya wengi.
“Hili ni swala lenye utata, tunafahamu kwamba mahakama imepiga marufuku uendelezwaji wa huu mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, lakini jambo la kushangaza ni kuwa mpapa sasa hivi kamati ya kitaifa ya nyumba ingali kuzunguka sehemu tofauti tofauti kukusanya maoni ya wakazi. Naomba mlizungumzie hili ili tulielewe vizuri.” alisema Nafula.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya kitaifa ya nyumba na aliyepia mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno, akitetea utendakazi wa kamati hiyo amesema mahakama imepiga marufuku utekelezwaji wa mswaada wa fedha wa mwaka 2023 wala sio swala la ukusanyaji maoni ya wakazi.
“Mahakama haijazungumzia swala la ukusanyaji maoni ya wakazi, Wakenya walienda kortini kujaribu kusimamisha ule mswaada uliopitishwa bungeni unaoitwa mswaada wa fedha wa mwaka 2023 na kufanywa kuwa sheria.
“Huo mswaada ulipitishwa kitambo sana takriban miezi minane iliyopita. Na ulipopitishwa ulikuwa unaongelea jinsi ya kukusanya ushuru kwa minajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu. Ndiposa Wakenya wakaenda kortini wakalalamika kuwa serikali inakusanyaje ushuru wa nyumba pasi kuwapo na sheria ya ujenzi?” alisema Ng’eno.
Aidha ameongeza kuwa uamuzi ulitolewa na mahakama juma lililopita ulilenga kusitisha ukusanyaji wa kodi itakayosaidia kugharamia ujenzi wa nyumba hizo za bei nafuu wala sio vinginevyo.
“Kwa hivyo mahakama ikasema huu ukusanyaji wa ushuru wa nyumba uendelee wakati kesi inasikilizwa wala sio wakati inaundwa sheria.
“Hiyo kesi ikaendelea Mkenya mwengine akarudi kortini akaomba kuwa ukusanyaji wa ushuru usitishwe wakati hii kesi inaendelea kusikizwa. Nayo mahakama ikasikiliza hiyo mpaka mwishowe, juzi ikaamua kwamba huo ukusanyaji ushuru usitishwe wakati kesi hiyo inaendelea.
“Tuje kwa hii yetu sasa haina uhusiano wowote na hiyo kesi iliyokuwa kortini.” alisema Ng’eno
Kamati hiyo ya kitaifa ya nyumba inatarajiwa kuzuru eneo bunge la Changamwe leo.