Maafisa wanne wa polisi waliokuwa wakisimamia kituo cha Muthaiga wakati ambapo mshukiwa wa mauaji Kelvin Kinyanjui Kang’ethe alitoroka kutoka kizuizini wamezuiliwa.
Katika taraifa kwa vyombo vya habari mapema Ijumaa, Kamanda wa Polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema kama mikakati ya kinidhamu ndani ya idara ya polsi, maafisa wengine wawili wa ziada wanaosimamia maafisa wanne husika wamehamishwa katika vituo vingine.
Aidha Bungei amefichua kuwa wakili wa Kang’ethe, John Ndegwa Maina anasalia kizuizini mwa polisi baada ya tukio hilo.
Maina alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga muda mfupi baada ya Kang’ethe kutoroka mwendo wa saa kumi na moja unusu jioni mnamo siku ya Jumatano.
Ukweli wa jukumu lake kama wakili wa Kang’ethe ulitiliwa shaka kufuatia kisa hicho hata hivyo Bungei akifichua kwamba uchunguzi wa awali umethibitisha utambulisho wake kama mwakilishi halisi wa kisheria wa mshukiwa.
Maina anaripotiwa kumtembelea Kang’ethe katika wadhifa wake kama Wakili wake mara nne kabla ya mshukiwa huyo kutoroka.
Ikumbukwe kuwa Kang’ethe anadaiwa kumwua mpenziwe wa umri wa miaka 31 mzaliwa wa Kenya huko mjini Whitman, jimbo la Massachusetts nchini Marekani na kisha kuutupa mwili wake kwenye gari katika uwanja wa ndege wa Logan jijini Boston mnamo mwezi Novemba mwaka jana.
BY MJOMBA RASHID