Baraza la Kikanda la Utawala wa Kazi Barani Afrika, (ARLAC) limekongamana hapa mjini Mombasa kujadili kwa kina mustakabali wa kikazi na ajira miongoni mwa wanachama wake.
Akihutubia kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Leba Florence Bore, mnamo Jumatano Februari 14, Katibu wa kudumu katika Wizara ya Leba na masuala ya jamii Shadrack Mwadime amesema suala la ukosefu wa ajira ni changamoto kuu inayokumba maeneo Mengi ya bara hili.
Kwa mujibu wa Waziri Bore, kuna haja ya washikadau wote wa baraza hilo kuungana ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zimetumika kubuni nafasi za ajira na kazi, na kuboresha mazingira ya kikazi ya wafanyakazi Barani Afrika ili kupunguza uhaba wa kazi.
“Ukosefu wa ajira ni mojawapo wa changamoto zinazolikumba Bara la Afrika kwa sasa licha ya uwepo wa nguvu kazi na ni hali ambayo inazuia matumizi ya rasilimali zilizopo. Inafaa tufanye uhamasisho wa matumizi bora ya rasilimali kwani mojawapo ya vigezo vya kukuza baraza hili lengo likiwa ni kubuni ajira kazi kwa wanachama,” alisema.
Katibu katika Wizara ya Leba na Masuala ya jamii, Shadrack Mwadime alitoa wito kwa wanachama wa ARLAC kuwatafutia wasio na ajira nafasi za kazi mataifa ya Ughaibuni akisema wana umilisi wa kutosha wa kufanya kazi katika mataifa ya Ugenini.
Mwandime alisema taifa la Kenya tayari limewatafutia Wakenya nafasi za ajira mataifa ya kigeni na hivi karibuni wanalenga kulipeleka kundi jingine litakalofaidika na mradi huo.
“Tunapeleka wafanyakazi wetu mataifa ya kigeni kwa sababu wana umilisi wa kutosha wa kutekeleza kazi za kitaaluma zilizoko ughaibuni. Viwanda na karakana za teknohama ughaibuni zinahitaji walio na ujuzi wa kutosha na umilisi wa kazi hiyo. Tumelitafutia kundi la kwa kwanza nafasi za ajira ughaibuni na hivi karibuni tunapeleka kundi jingine mataifa ya kigeni,” alisema Mwadime.
Mwenyekiti wa baraza hilo July G. Moyo alitoa wito kwa wanachama kutoa mafunzo ya umilisi kwa washikadau wote katika sekta ya leba ili kuboresha sekta hiyo na kutoa uongozi bora katika mataifa yao.
“Kufikia sasa tumetoa mafunzo ya umilisi kwa maafisa na wataalamu wa masuala ya leba baadhi ni wa kiserikali na wengine wametoka katika mashirika ya kibiashara. Hawa ndio wanashika usukani katika wizara za leba kulihudumia taifa lao kutumia ujuzi waliopata kutokana na mafunzo kama haya.” Alisema.
Kuandaliwa kwa Kongamano hilo kunafikisha Maadhimisho ya 50 ya Baraza hilo mwaka huu 2024, Kauli mbiu ikiwa ni: ‘Kutoa umilisi kwa Wafanyakazi ili wawe na stadi za kazi na ushindani wa Kimataifa katika maendeleo na ajira endelevu.’
BY NEWSDESK