HabariLifestyleNews

Wizara ya Usalama wa Ndani na Hospitali ya Kenyatta Zaongoza kwa Wafanyakazi Wenye Vyeti Ghushi

Imebainika kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ndizo zinaongoza kwa idadi ya wafanyakazi walio na vyeti ghushi.

Tume ya Huduma za Umma, PSC imefichua kuwa kuna idara mbalimbali muihmu za serikali ambazo zinaongoza kwa wafanyakazi waliopata nyadhfa hizo kwa kutumia vyeti ghushi.

Kulingana na tume hiyo, Ufichuzi huo wa kushangaza uliotolewa unaonesha kuwa wengi wa wafanyakazi walioghushi vyeti ili kupata kazi mbalimbali ni katika Wizara ya usalama wa Kitaifa na masuala ya ndani, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi, Shirika la Geothermal Development ambalo liko chini ya Wizara ya Kawi.

Akihutubia wanahabari mnamo Jumanne, Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Huduma za Umma, Balozi Anthony Muchiri alisema watu hao ni sehemu ya visa 2,067 vya kughushi vyeti ambavyo walichunguza katika zoezi walilolianzisha mnamo mwezi Oktoba 2022.

Uchunguzi huo ulilenga taasisi 331 miongoni mwao ni Wizara na Idara za Kiserikali 52 na mashirika ya kiserikali 239 pamoja na vyuo vikuu vya umma 40.

Katika uchunguzi huo taasisi hizo zilihatija kutoa orodha za wafanyakazi wake waliofuzu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, katika kila mwisho wa mwaka na pia kuipa tume idhini ya kufikia na kuthibitisha mtandaoni vyeti vya kitaaluma vya watahiniwa wanaotafuta kazi.

BY MJOMBA RASHID