Serikali kupitia Wizara ya Usalama wa ndani ya nchi imefutilia mbali leseni ya baa, migahawa na vilabu vya mvinyo vinavyohudumu maeneo ya makazi na karibu na shule.
Waziri wa usalama wa ndani na masuala ya kitaifa Prof. Kithure Kindiki mnamo siku ya Jumatano alitangaza kuwa leseni tayari zilizopeanwa na serikali za kaunti ambazo ni kinyume cha sheria ya kudhibiti vinywaji vya pombe, hasa katika makazi ya watu na maeneo ya taasisi za elimu zimebatilishwa na hazifai.
Waziri Kindiki aidha alitangaza kuwa wamiliki wa nyumba na majengo watawajibishwa kwa kuruhusu baa na vilabu kukodisha nyumba kuendesha shughuli kwenye maeneo hayo ambayo yalipigwa marufuku.
“Wamiliki wote wa nyumba na wamiliki wa majengo watachukuliwa kuwa wasaidizi na watawajibishwa kwa kukodisa nafasi kwa ajili ya kuanzishwa baa/Vituo vya mvinyo na vinywaji vikali katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kwa mujibu wa kifungu cha 20 (c) cha Kanuni ya Adhabu,” alisema Waziri huyo.
Alitoa miongozo mipya inayosimamia uuzaji dawa na pombe nchini akisema kuwa uraibu wa dawa za kulevya na matumizi ya pombe haramu ni tishio kwa usalama wa kitaifa.
Kwa sasa amewaagiza wakuu wa usalama wa kaunti kufunga na kusimamia majengo hayo kuhakikisha yanasitisha utoaji huduma hizo mara moja.
Wakati uo huo Waziri Kindiki amelitaka bunge kufanikisha marekebisho ya sheria inayokabili udhibiti wa dawa na pombe nchini ili kusaidia kukabili Donda sugu la ulanguzi wa mihadarati.
Amesema kurekebishwa kwa sheria hiyo kutahakikisha kuwa utoaji wa leseni za kibiashara za dawa na pombe katika ngazi za kaunti kunafanyika tu baada ya kuidhinishwa na Mamlaka ya Kukabilia matumizi ya dawa na pombe, NACADA.
“Bunge linatakiwa kulipa kipaumbele na kuharakisha kufanyika mchakato wa kuingilian kati kwa bunge hasa mageuzi kwa Sheria ya Kukabiliana na Pombe, na kuhakikisha kuwa utoaji wa leseni wa kaunti unafanyika ni kwa masharti ya kuuidhinishwa na NACADA kabla ya kuuza au kusambaza,” alisema.
Zaidi ya hayo serikali imesitisha leseni kwa watengenezaji wote wa pombe ya awamu ya kisasa na watahitajika kutuma maombi mapya ndani ya wiki tatu vilevile imesema kuwa leseni zote halali zitahakikiwa upya ndani ya siku 21.
BY MJOMBA RASHID