HabariLifestyleMombasaNews

Serikali ya Kaunti ya Mombasa Yafungua Kituo cha Hifadhi na Matibabu ya Watoto Wachanga waliozaliwa kabla ya Muda

Huduma za afya hasa kwa watoto kaunti ya Mombasa zinatarajiwa kuimarika zaidi kufuatia ufunguzi wa kituo kipya cha matibabu kwa watoto wachanga ‘New born Unit’ katika hospitali ya Port-Reitz eneobunge la Changamwe.

Kituo hicho maalum kilichojengwa kwa ushirikiano wa kampuni ya mafuta ya Kenya Pipeline, shirika la KEMSFED kupitia SCAF Kenya Pamoja na serikali ya kaunti ya Mombasa kinatarajiwa kutoa matibabu kwa Watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati na wale wenye matatizo ya kiafya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kituo hicho mnamo sku ya Alhamisi, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir amesema kuwa kituo hicho kitapiga jeki huduma za afya hasa kwa wakazi wa eneo hilo na kuwapunguzia gharama na mahangaiko ya kusaka huduma za afya.

Gavana Nassir amesema hospitali zote za umma kaunti hiyo zitafanyiwa marekebisho na kuwezeshwa na vifaa vya kisasa vya matibabu ili kuboresha utoaji huduma za afya mashinani na kupunguza msongamano katika hospitali Kuu ya Makadara.

“Hospitali zetu zitafanyiwa marekebisho ikiwa pamoja na hii na iko katika mpangilio wa kuweza kufanyiwa marekebisho ya eneobunge la Changamwe ikiwemo kuweka majenereta,kuweka ukuta na kuzifanya ziwe za masaa 24.” Alisema Gavana Nassir.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa kampuni wa Kenya Pipeline, Joe Sang alisema wataendelea kushirikiana na serikali ya kaunti ya Mombasa ili kufanikisha hatua hizo.

“Kama kampuni ya Kenya Pipeline tutaendelea kushirikiana na serikali ya Mombasa na mawakilishi wadi pia wanafanya kazi nzuri na serikali kuu pamoja na serikali ya kaunti pia tutashirikiana  ili kuhakikisha hatuka nyuma ya Pipeline.” Alisema.

BY NEWSDESK