Mwenyekiti wa Bandari ya Lamu, LAPSSET, Ali Menza Mbogo ameeleza haja ya kuimarisha kwa mazingira katika fuo za bahari katika ukanda wa Pwani ili kuongeza mapato na kukabiliana na mabadiliko ya hewa.
Akizungumza mnamo Jumamosi katika uwanja wa Basra-Manyani huko Mishomoroni eneo bunge la Kisauni baada ya zoezi la Upanzi wa miti aina ya mikoko kwenye ufuo wa Manyani ‘Manyani Beach,’ Mbogo alieleza haja kwa wakaazi na viongozi wa eneo hilo kushirikiana ili kuhakikisha fuo katika eneo hilo zinakuwa safi kwa ajili ya .
Mbogo ambaye alikuwa Mbunge eneo hilo amebainisha kuwa zoezi hilo sio la kisiasa na kuahidi kuungana na viongozi wengine ikiwemo mwenyekiti wa Mamlaka ya Bandari, KPA Benjamin Tayari na Mwenzake wa Mamlaka ya Ubaharia (KMA) Hamisi Mwaguya kuunga juhudi za kuhakikisha mazingira hasa katika fuo yanakuwa salama kwa faida ya viumbe wa baharini na wakaazi.
“Mimi kama chairman wa Lapsset, Chairman ndugu yangu Mwaguya wa KMA na nitajaribu pia Chairman wetu wa KPA, muheshimiwa Bemjamin Tayari pia tumlete pia katika hii shuhuli ili tuweze kuungana kama viongozi wa pwani tuhakikishe tunaskuma gurudumu hili mbele, lakini kwanza hadi tuhakikishe kuwa sisi kama wenyeji hapa tunachukua jukumu kutunza mazingira,” alisema Mbogo.
Wakati uo huo Mbogo alionyesha kusikitishwa kwake na changamoto ambazo zimekumba eneo hilo hasa msitu wa Manyani unaozunguka ufuo wa bahari hiyo kutumika kama choo na wakaazi wengi ambao wamekosa raslimali na sehemu za kwenda haja, kuwa miongoni kuwa sababu zinazochangia uchafu wa bahari.
“Niwape historia kwa nini tangu tukiinukia hadi sasa ikaitwa ‘Mavimavi Beach’ ni kutokana na wakazi kukosa vyoo wakati huo waliona sehemu ya kwenda ni msituni na baharini hapa na hadi sasa hali bado iko hivyo nimesikitishwa na chifu wa eneo hili alivyosema kuwa kuna watu wanaoenda msituni kujisaidia hadi sasa, inabidi hili libadilike jamani,” alisema.
Hata hivyo amepongeza juhudi za shirika la Akili Kadhaa za kusafisha bahari akiahidi kuunga mkono juhudi hizo na kukabiliana na changamoto zinazokumba eneo hilo.
“Ajenda kuu ni kuboresha mazingira yetu yah ii bahari ambayo famously inajulikana kama mavimavi beach, katika karne ya leo bado kuna sehemu hapa manyani hazina vyoo, na ikiwa mtu hana choo na yuko karibu na bahari, basi mahali anapoweza kuenda kujisaidia ni pale katika msitu wa bahari.
Lakini tuna imani kupitia CBO yetu ya Akili Kadhaa ambao wamejitolea kupitia viongozi kama sisi tunasimama na wao tuhakikishe tumeboresha bandari yetu hii ya hapa.” Aliongeza Mbogo.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa shirika hilo Juma Mashuhuri, amesema Wanashirikiana na vitengo mbalimbali vya usimamiz wa fuo eneo hilo kuhakikisha fuo za bahari zinakuwa safi.
Mashuhuri ameongeza kuwa wameweka mikakati ya kuihamasisha jamii ya eneo hilo kuhusu umuhimu wa kuyalinda mazingira ya bahari kwa faida ya watumizi wote hususan wavuvi ambao wanategemea uvuvi wa samaki eneo hilo kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.
“Mikakati ni kwamba ni kuweza kuleta wana vijiji wote kwanza kuweza kuwapa ile awereness kwamba umuhimu wa usafi wa hii bahari kwa kiasi gani inaweza kuwasaidia wao na jinsi gani tunaweza kuieka safi kwa ajili ya afya zetu ya sisi na kizazi cha baadaye.” Alisema Mashuhuri.
Shughuli hiyo iliyosimamiwa na Shirika la Kijamii la Akili Kadhaa kwa ushirikiano na washikadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Baharini, KMA na KEMFRI ilishuhudia usafishaji wa ufuo wa bahari wa Manyani sawia na upanzi wa miti ya mikoko zaidi ya 500 katika awamu ya kwanza ya mradi huo.
Awamu ya kwanza ya mradi huo unatekelzwa kwa kipindi cha miezi sita.
BY (MJOMBA) RASHID R. ALI