HabariNews

Vikaragosi wa Siasa! Spika Amason Kingi Aapuuzilia mbali wito wa Umoja wa Viongozi wa Pwani

Spika wa Bunge la Seneti Amason Jeffa Kingi ametilia shaka wito wa muungano wa viongozi walioko katika vyama tofauti vya kisiasa kushinikiza ajenda za maendeleo eneo hili.

Akizungumza katika hafla sawia Kingi amesema wito wa umoja wa viongozi umekuwa kwa muda mrefu pasi maafikiano huku akipuuzilia mbali uwezekano wa kuafikiwa maendeleo kwa viongozi kuendelea kusalia katika vyama vingine.

“Sioni mafanikio hapa mnataka kusukuma maendeleo kuungana na kila mmoja yuko katika chama kingine, ODM na wengine UDA kivipi tutaweza kusukuma umoja na kutafuta uongozi wa 2027? Ni hadi muwe ndani ya chama kimoja.” Alisema.

Kingi aliyepia mwanzilishi wa chama cha Pamoja African Alliance, (PAA) amewataka viongozi wa Pwani kuepukana na utumwa wa kisiasa kwa kushabikia viongozi na vyama vingine vya kisiasa.

“Tumekuwa tukiimba wimbo huu kwa miaka nenda miaka rudi zama za kina Ngala, wakati nikisoma hadi sasa, lakini shida sisi ni vikaragosi wa siasa tunachezeshwa na viongozi wanavyotaka, ikiwa hatutabadili mwamko wa kushabikia vyama vingine basi ni kazi bure…” alisema.

Kingi alkiyekuwa Gavana wa Kilifi pia aliwataka viongozi hao kujiunga na chama cha PAA ambacho kiliundwa kwa ushirikiano wa viongozi wote wa Pwani kabla ya wengine kukigura na kujiondoa chamani.

“Uzuri nyinyi nyote hapa viongozi mlishiriki na tulikuwa pamoja kuunda PAA mnajua viruzi nilkuwa na malengo hasa na nyinyi pia kwa dhati tulitaka kuunganisha, lakini sasa inakuaje tushinikize maendeleo tukiwa vyama tofauti? Alisema.

Kingi vile vile aliwasihi Wapwani kuunga mkono serikali kwa ajili ya maendeleo na manufaa zaidi ya miradi mbalimbali na uongozi.

“Hatuwezi kushinikiza serikali itufanyie maendeleo na mambo mengi ilhali hatukumpa kura za kutosha kama maeneo mengine, ni sasa tushikane tumpe William Ruto aslimia 90 katika kura za 2027.” Alisema.

BY MJOMBA RASHID