Brigedia Swaleh Said ni miongoni mwa maafisa wakuu wa jeshi walioaga dunia hapo jana kufuatia ajali ya ndege ya kijeshi iliyoua wengine 9 akiwemo mkuu wa Majeshi Francis Ogolla.
Biwi la simanzi limetanda katika familia yake Brigedia huyo katika eneo la Utange Shanzu kaunti ya Mombasa.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha radio, mamaye Brigedia Said, Saada Soud Mahmoud ameutaja msiba wa mwanawe kama pigo kubwa kwake na familia nzima.
Saada amemtaja mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka 56 kuwa tegemo kubwa kwa familia yake na kwamba ataishi kukumbukwa.
“Nimeondokewa na mtu wa maana sana kwangu, mshauri wangu wa karibu. Ana radhi yangu simsifu kwa kuwa ni mwanangu lakini…sina la kusema…” alisema.
Bi. Saada amemtaja mwanawe Brigedia Said kuwa mpole, mchapa kazi aliyetangamana na kuenziwa na maafisa wenzake wakubwa kwa wadogo katika jeshi.
Alieeleza nyakati za mwisho kuzungumza na mwanawe na kabla ya kifo chake Alhamisi Aprili 18, kuwa alitamani sana kuzungumza naye lakini kila alipojaribu hakumpata kwenye simu.
“Siwezi kushindana na amri ya Mungu na ahadi imefika nilitarajia mwanangu anizike kumbe ndio nitamzika, ni majaliwa pia siwezi nikakufuru kushindana na amri ya Mungu.”
Brigedia Swaleh Said alisomea shule ya msingi ya Utange eneo la Shanzu kaunti ya Mombasa na baadaye kujiunga na shule moja ya Upili eneo la Thika, kabla ya kujiunga na jeshi la ulinzi, KDF.
Marehemu Brigedia Said ameratibiwa kuzikwa leo jioni baada ya swala ya Alasiri kwa mujibu wa kanuni za dini ya Kiislamu.
BY NEWS DESK