HabariLifestyleNews

NACADA Yaagiza Kufungwa kwa Baa Zilizo Karibu na Taasisi za Masomo Nchini

Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Pombe na Mihadarati NACADA imeagiza kufungwa mara moja kwa baa na vilabu vinavyohudumu karibu na taasisi za masomo nchini.

NACADA sasa imetangaza oparesheni ya kitaifa dhidi ya baa na vilabu vinavyohudumu karibu na taasisi za elimu kwa mujibu wa sheria ya kudhibiti Pombe ya mwaka 2010.

Kwa mujibu wa sheria hiyo vilabu na baa zinapaswa kuweko umbali wa mita 300 kutoka shule za chekechea, msingi, sekondari, au katika taasisi zozote za elimu zinazohudumia watu chini ya umri wa miaka 18.

Kulingana na agizo hilo la NACADA lililotolewa mnamo Jumatatu Mei 27, watakaokiuka sheria hiyo wanakabiliwa na adhabu itakayojumuisha faini isiyozidi shilingi 500,000, kifungo gerezani kisichozidi miaka 3 au yote hayo mawili.

Oparesheni hiyo ya NACADA itahusisha ushirikiano wa idara husika za kitaifa na za kaunti kuhakikisha kuwa taasisi hizo za vileo zinazingatia sheria.

Ikumbukwe kuwa agizo hilo la NACADA linajiri wiki moja tu baada ya Mamlaka hiyo kuagiza kuondolewa kwa mabango ya kutangaza biashara za vileo karibu na taasisi za elimu kote nchini.

BY MJOMBA RASHID