Habari

Mshukiwa wa mauaji ya msichana wa miaka 8 kuendelea kuzuiliwa………

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kinyama ya msichana wa miaka minane, Shantel Nzembi, atazuiliwa kwa siku saba zaidi huku uchunguzi ukiendelea.

Navity Mutindi atazuiliwa katika gereza la kitengela baada ya mahakama ya Kajiado kukubali ombi la upande wa mashtaka ambao umesema unalenga kufanikisha uchunguzi.

Mutindi amefikishwa mahakamani akiwa na mshukiwa mwenzake Patrick Mureithi, japo wote hawakuitikia mashtaka waliyosomewa.

Wakiwa mbele ya hakimu mkaazi wa Kajiado Edwin Mulochi, mahakama iliambiwa kwamba Mureithi alisajili laini ya simu ambayo ilitumika kuitisha kikombozi cha shilingi elfu 300 kutoka kwa mamake Shantel Christine Ngena baada ya kutoweka nyumbani kwao katika eneo la Kitengela.

Kufikia sasa washukiwa wanne wamefikishwa mahakamani kufuatia mauaji hayo ya Shantel.

Shantel alipotea jumapili iliyopita na kupatikana akiwa ametupwa huku ikiarifiwa kwaba huenda alibakwa kabla ya kuuawa.

 

By Warda Ahmed