Habari

Polisi Msambweni wachunguza kifo cha mwanafunzi wa chuo kikuu…….

Polisi huko Msambweni katika kaunti ya Kwale wanachunguza chanzo cha kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya huko Thika  aliyezama kwenye kidimbwi cha kuogelea katika hoteli moja eneo la Diani.

Mwendazake kwa jina  Stephen Omondi mwenye umri wa miaka 28, amezama maji katika hoteli ya Safari Beach akiogelea alipokuwa pamoja na wanafunzi wenzake 17.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi kaunti ya Kwale Ambrose Oloo amesema wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mount Kenya walikuwa wakifanya masomo yao ya kawaida hadi baada ya chakula cha mchana walipoamua kuogelea kwenye kidimbwi hicho.

Marehemu aliripotiwa kuaga dunia baada kuwasili katika hospitali ya Diani.

Mkasa huu unajiri juma moja tu baada ya mapacha kuzama katika baharini katika eneo la Gazi huko Msambweni walipokuwa wamekwenda kumtembelea babayao baada ya kumaliza masomo yao ya kidato cha nne.

Kamanda huyo wa Polisi amewataka wageni kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na usimamizi wa hoteli wakati wa kuogelea kwa usalama wao.