HabariNews

FAMILIA MOJA KILIFI KASKAZINI YAWAOMBA VIONGOZI NA WAHISANI KUWASAIDIA KULIPA DENI KATIKA HOSPITALI YA KITAIFA YA KENYATTA.

Familia moja kutoka kijiji cha Kibokoni eneo bunge la Kilifi kaskazini imewaomba viongozi na wahisani kujitokeza na kuwasaidia kulipa deni katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi ili waweze kupewa mwili wa mpendwa uliozuiliwa hospitalini humo kufuatia kushindwa kulipa deni hilo.

Wakiongozwa na Sulubu Mangi, ambaye ni baba wa marehemu Sophie Kadzo, deni hilo la takriban shilingi milioni moja linatokana na marehemu kupewa matibabu ya saratani ya koo aliyokuwa akiugua.

Hata hivyo familia hiyo imeeleza kuwa changamoto ya kulipa deni hilo imechangiwa na wao kuuza mali zao ili kumtafutia matibabu mpendwa wao, hali iliyowapelekea wao kusalia bila chochote.

Kwa upande wake Kitsao Kambi mjomba wa marehemu ametoa wito kwa viongozi kaunti ya Kilifi kutafuta mbinu ya kuwasaidia kwa kufanya mazungumzo na usimamizi wa hospitali hiyo ili deni lao lifutiliwe mbali, na waweze kupewa mwili wa mpendwa wao wakauzike.

BY EDITORIAL DESK