AfyaGadgetsHabariKimataifaLifestyleNews

Afueni kwa Wajawazito nchini, Majaribio ya Kifaa Maalum cha kupima kiwango cha damu wakati wa kujifungua yakishika kasi.

Wanawake hapa nchini sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya majaribio ya kifaa cha kupima kiwango cha damu wanawake hupoteza baada ya kujifungua yakiendelea kushika kasi.

Afisa mkuu wa matibabu katika hospitali ya Malindi kaunti ya Kilifi David Ng’ong ameutaja uzinduzi huo kuwa unalenga kupunguza idadi ya vifo vya akina mama vinavyotokana na uvujaji damu wakati wa kujifungua.

“Kifaa hiki kinatumika kupima damu ambayo mjamzito amevuja. Kama damu imepita kiwango ambacho daktari ataona mama anahitaji kuongezewa damu ifanyike kwa wakati unaofaa na kuokoa maisha yake,” akasema Bw. Ng’ong.

Ng’ong anasema kifaa hicho ambacho kinafanyiwa majaribio kitawasaidia wanawake kupata damu ya kutosha baada ya kujifungua.

Afisa huyo aidha amebainisha kuwa kifaa hicho kitasambazwa kote nchini punde tu kitakapo idhinishwa ili kitumike na wizara ya afya.

Tayari kifaa hicho kimewasaidia takriban wanawake 6,000 katika hospitali ya Malindi kaunti ya Kilifi wakati wa kujifungua.