HabariNews

‘Kaunti za Pwani zina kila sababu ya Kujivunia Ugatuzi,’ Seneta Miraj

Kaunti za pwani zina kila sababu ya kujivunia ugatuzi tangu kuanzishwa kwake miaka kumi iliyopita.

Seneta mteule Miraj Abdillahi amepongeza hatua ugatuzi ulipofikia akisema kwamba umesaidia akina mama kwa kiasi kikubwa kunufaika na huduma mbalimbali kwa haraka zikiwemo maji na matibabu.

Akiongea huko mjini Eldoret kwenye Kongamano la Ugatuzi linaloendelea Miraj alisema kupitia ugatuzi, hospitali nyingi zimeweweza kupata vifaa mwafaka vya matibabu na kuwa wakazi wa Pwani wanapata huduma bora za matibabu kwa urahisi kutokana na kugatuliwa kwa huduma za afya.

 

“Ugatuzi umeleta mafanikio na maendeleo mengi Pwani, sasa hivi akina mama wanapata huduma bora za afya tena kwa urahisi. Kwa sababu sisi kina mama huwa wa kwanza kuathirika sana na ukosefu wa huduma za msingi kama maji na matibabu,” alisema Miraj.

Wakati huo huo Miraji ameeleza kujivunia mpango maalum wa Rais William Ruto na gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharif Nassir kuhakikisha kuwa mabomba ya zamani ya maji yalibadilishwa kuhakikisha kuwa wakaazi wa kaunti hiyo wanapata maji safi.

“Nimpongeze rais wangu William Samoei Ruto kwa ushirikiano na gavana wa Mombasa kuhakikisha mabomba yale ya zamani yam aji yanabadilishwa ili wananchi wetu wa Mombasa wapate huduma hiyo kwa urahisi, n ahata kote nchini rais ameonyesha uongozi na utekelezaji wa ahadi na miradi yake,” akaongeza Miraj.

Wakati huo huo Seneta huyo mteule ametoa wito wa kugatuliwa kwa huduma zote za msingi ili msaada uweze kufikia mwananchi wa kawaida kwa haraka na urahisi.

BY MJOMBA RASHID