HabariNews

Vijana na Wanawake wakosa kuhusishwa kutokana na ukosefu wa elimu ya Tabia nchi

Ukosefu wa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi miongoni mwa wanawake na vijana umetajwa kuwapelekea kutohusishwa kikamilifu katika maswala ya mabadiliko ya tabia nchi.

Afisa wa Maswala ya mabadiliko ya tabia nchi Nancy Cheki kutoka shirika la Young Women Christian Association YWCA alisema mara nyingi vijana na wanawake huachwa nyuma katika maswala hayo kutokana na ukosefu wa elimu  sasa akiwataka wanawake na vijana kuhusishwa kikamilifu.

Aidha Cheki  aliongeza kusema kuwa, maswala  ya mabadiliko ya  tabia nchi huathiri kila mmoja wakiwemo vijana na wanawake akionyesha  haja ya wao  kuhusishwa ili kutoa maoni yao na  changamoto zinazowakabili.

“Swala ambalo limejitokeza ni ukosefu wa elimu ambayo imekuwa chanzo cha wanawake na vijana kukosa kuhushishwa katika maswala haya ukimpa mwanamke elimu unamwezesha aweze kutoa maoni yake na changamoto na hapo anaweza kutoa suluhisho ya matatizo yanayokumba idara hiyo.”Alisema Cheki.

Cheki aidha, alipongeza hatua ya viongozi waliohusika katika maandalizi ya kongamano linaloendelea jijini Nairobi kwa kuhusisha wanawake na vijana akisema idadi ya wawakilishi waliofika kwenye kwenye kongamano hilo ni ya kuridhisha .

Kulingana na Cheki kumekuwa na changamoto za kimitambo katika usajili akitoa wito kwa asasi husika kushughulikia swala hilo haraka iwezekanavyo.

“Ukiangalia uwakilishwaji wa vijana na wanawake kwenye hili kongamano ni wengi sana japo kumekuwa na changamoto za kimitambo katika kupata ruhusa ya kuingia ndani pengine waweze kushughulikia swala hili kwa uharaka ili wapunguze msongamano wa watu.”Alisema.