HabariNews

Ajali 2 ZAUA Watu 20 Barabara kuu ya Nairobi – Mombasa

Watu 20 waliaga dunia na wengine wakijeruhiwa kufuatia ajali mbili tofauti barabarani ndani ya muda wa saa 24 zilizopita katika barabara kuu ya Mombasa – Nairobi.

Wanane kati yao waliaga dunia usiku wa kuamkia Ijumaa katika eneo la  Mlima Kiu kaunti ya Makueni. Akithibitisha ajali hio iliyotokea mwendo wa saa tano usiku, Kamishna wa polisi Makueni Barbanas Ng’eno, alisema kuwa wanane hao walifariki papo hapo baada ya matatu walikuwa wameabiri kugongana ana kwa ana na lorry.

Miili ya walioaga ilipelekwa katika hospitali ya Kilungu huku mabaki ya gari yakifikishwa katika kituo cha polisi cha Salama.

Hali kadhalika watu 12 walifariki katika barabara iyo hiyo kuu eneo la Ndii huko Voi kaunti ya Taita Taveta. Akithibitisha ajali hiyo Mkuu wa polisi eneo la Voi Bernstein Shari, alibaini kuwa watu hao waliaga dunia baada ya Matatu waliokuwa wakisafirira kugongana na Lorry ana kwa ana  Alhamisi Septemba 7 mnamo mwendo wa saa kumi alasiri.

Majeruhi walifikishwa kupokea matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi huku uchunguzi kubaini tukio hilo ukianzishwa.

Ajali hizi zimetokea sawia katika barabara moja na chini ya saa 24 zimeibua hofu kwa wasafiri huku maderewa wakitakiwa kuwa makini hasaa wanaobeba abiria.

BY EDITORIAL DESK