HabariNews

Mahakama ya Kadhi Iheshimiwe na iwe na Uamuzi wa Mwisho, Viongozi Wasema

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Dor alieleza haja ya Afisi ya Kadhi Mkuu kupewa mamlaka ya kuiwezesha kutoa uamuzi wa mwisho kwa masuala yote yanayofungamana na waislamu.*

Akiongea katika Dhifa la kumkaribisha kadhi Mkuu Sheikh Abdulhaleem Athman, Sheikh Dor alisema kesi zote zinazohusu dini ya kiislamu zinafaa kuamuliwa na mahakama ya kadhi pasipo kuamuliwa au hata kukatwa rufaa katika mahakama yoyote isiyokuwa ya kadhi.

“Makadhi wako wote bwana Chief Kadhi wapewe elimu, civic education umuhimu wa kusema kwa kauli moja pasi migongano. Kisha afisi yako iwe imara iwe waislamu hatuna budi ni lazima tutumie mahakama ya kadhi na tuwe na uaminifu kwamba uamuzi ukitoka hakuna haja ya kwenda mbele,” alisema Sheikh Dor.

Naye Kadhi mstaafu Sheikh Ahmed Shariff Muhdhar alipongeza juhudi za SUPKEM kusimamia masuala mbalimbali yanayohusu waumini.

“Mimi binafsi niliwahi kunufaika na ufadhili wa masomo mwaka wa 1979 kusomea nje ya nchi na nashukuru sana Supkem. Hivyo nina imani hadi leo hii kwa ushirikiano na viongozi hawa masuala ya waislamu yatapata nguvu serikalini,” Alisema.

Katika hafla hiyo Maafisa wa masuala ya Ndoa katika Afisi ya Kadhi walitoa wito wa kuharakishwa kwa mchakato wa vyeti vya ndoa wakilalamikia changamoto ya ukosefu na ucheleweshwaji wake suala walilolitaja kuchangia ugumu katika kutelekeza majukumu yao ipasavyo.

“Waislamu tujue kwamba cheti cha ndoa hapa Kenya imekuwa sawa na kitambulisho, lazima aliyeoa awe na cheti chake leo. Mimi mwaka wa pili sasa imekuwa kitabu cha vyeti vya ndoa kikimalizika nalazimika kukaa miezi 6 kusubiri kitabu. Kadhi mkuu hii naomba afisi yako ishughulikie,” alisema mmoja wa maafisa hao.

Naye Mohammed Jaffar Mfanyabiashara mashuhuri wa Kampuni ya Grain Bulk Handlers aliitaka Afisi ya Kadhi kuangazia changamoto za vijana kwa kuweka mikakati mwafaka ya kuwaendeleza kuwanasua katika lindi la mihadarati.

Bw. Jaffar aidha alihimiza Afisi ya Kadhi na viongozi wengine wa Kidini kulipa umuhimu suala la mitandano kwa kuwekeza katika kutoa mafunzo ili isitumike vibaya kuwapotosha vijana.

“Bwana Chief Kadhi vijana wengi wetu wanaangamia na dawa za kulevya na hii mitandao sasa hivi kama tiktok imekuwa hatari, tusipofanya jambo tutapoteza umma na jamii yetu,” Alisema.

Dhifa hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kidini, mawaziri wa kaunti ya Mombasana viongozi wengine wa kijamii na Wafanyabishara mashuhuri miongoni mwa wageni wengine waalikwa.

BY MJOMBA RASHID