HabariNewsSiasa

Odinga amsuta Gachagua, akariri msimamo wa AZIMIO kwenye mazungumzo ya Kitaifa

Kinara wa muungano wa Azimio la umoja-one Kenya Raila Odinga amekariri msimamo wa muungano huo kuhusu ajenda zake kuu kujadiliwa kwenye mazungumzo ya maridhiano.

Akiongea kwenye mahojiano na kituo cha runinga ya KTN News Odinga amesema kwenye ajenda zao masuala ya uchaguzi wa haki na gharama ya maisha limekuwa mstari wa mbele kwenye mazungumzo ya kitaifa yanayoendelea katika Ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.

Odinga aidha amesema suala la kufanyiwa mageuzi kwa baadhi ya vipengee vya katiba, kuimarishwa kwa demokrasia ya vyama vingi pamoja na uhuru wa vyama vya kisiasa ni miongoni mwa ajenda muhimu ambazo kamati hiyo inapaswa kuziangazia.

Kubwa ya ajenda zetu ilikuwa ni gharama ya maisha, hilo lilikuwa letu la kwanza, tulitaka suala la gharama ya maisha kuwa hapo, pili suala la uchaguzi wa haki kuwa hapo na tatu tulitaka demokrasia imara ya vyama vingi kusiwe na uingiliaji wa vyama vya kisiasa iwe hapo kisha tulitaka yale marekebisho mengine ya katiba,’ alisema Odinga.

Wakati uo huo Odinga amemsuta vikali Naibu rais Rigathi Gachagua kwa semi zake za kupuuzilia mbali mazungumzo ya kitaifa na kuitaja nchi kama kampuni akimtaja Gachagua kama mbinafsi asiye na mwelekeo na kiongozi anayeitia nchi aibu.

Raila aidha alisema kuwa matamshi kama hayo aliyoyatoa naibu rais si ya heshima na hadhi kama kiongozi wa cheo chake hicho.

Maneno kama hiyo kwa mtu kama yeye tena kiongozi ni aibu na kuleta chuki. Akiongea anasema wao na sisi…na tena anasema Kenya ni kampuni ambayo ina hisa; kuna wengine wana hisa zaidi, wengine wana hisa chache, wengine hawana chochote. Hiyo inaweza kugawanya nchi.” Alisema.

Raila aliendelea kumsuta Gachagua na akimtaja kama kiongozi anayebagua baadhi ya maeneo ya taifa akidai kuwa hastahili kuwa kiongozi.

Huyo bwana Gachagua nimesema ni mtu ambaye hastahili awe naibu wa rais wa taifa, maanake mdomo yake ni chafu; anatoa maneno ambayo inaweza kuleta mapigano katika taifa. Yeye inasemekana ni naibu wa rais wa taifa la Kenya, lakini anajifanya kama yeye ni naibu wa rais wa mlima Kenya, pande zingine za Kenya ni kigeni kwake,” alisema Odinga.

 BY EDITORIAL DESK