HabariNewsTravel

KWS yawataka Wageni wanaozuru Fuo za Bahari mjini Malindi kuzingatia sheria

Wageni wanaotembelea maeneo ya fuo za bahari ukanda wa Pwani wametakiwa kuzingatia sheria za ufuoni ili kukwepa kukabiliwa na mkono wa sheria.

Shirika la huduma za Wanyamapori nchini KWS mjini Malindi kaunti ya Kilifi lilitoa tahadhari kwa wageni wanaoendeleza ziara zao kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria za eneo hilo kikamilifu.

Afisa Mkuu msimamizi wa Shirika hilo mjini humo Ntindi Kassim alisema kuwa sheria zinapaswa kuzingatiwa hasa katika maeneo ya hifadhi sawia na maeneo mengine huku akiwataka wazazi kuwa makini na watoto wao wanapuzuru maeneo hayo.

 

Zile familia ama wageni ambao watakuja katika fuo zetu za bahari tunawaomba wakati wanakuja kule chini wafuate sheria, pili wakiandamana na watoto wahakikishe wako na watoto kwa karibu,” alisema.

Afisa huyo alisema tayari KWS imeweka maafisa wa kutosha walio na ujuzi na masuala ya uokozi wakati wa dharura akihimiza wakazi kuondoka maeneo ya ufuoni mara moja inapotimu majira ya saa kumi na mbili jioni.

 

Tuna maafisa wetu tumeweka kule ufuoni ambao wamepitia mafunzo ya kusaidia wakati kuna mkasa. Na tunawausia waweze kuondoka, baada ya saa kumi na mbili jioni watu wote wawe wametoka kwa fuo za bahari kwa usalama wao,” alisema.

Wakati uo huo afisa huyo alisisitizia umuhimu wa ushirikiano wa wakazi wa eneo hilo na idara hiyo katika uhifadhi wa asasi na raslimali za baharini, ili kuhakikisha shughuli za baharini zinatekelezwa pasi changamoto.

BY NEWSDESK