HabariNews

Shule ya Upili ya Wasichana ya St. Johns Kaloleni, Yafungwa kwa Siku wa 4.

Usimamizi wa shule ya Wasichana ya St. Johns Kaloleni umeamua kuifunga shule hiyo kwa muda wa siku 4, huku wanafunzi wote wakirejea majumbani.

Kufungwa kwa shule hiyo ni kutokana na kuchomeka kwa bweni la shule hiyo usiku wa Jumatano wakati wanafunzi walipokuwa madarasani kwa masomo.

Shule hiyo ya upili ya bweni ilifungwa kuanzia mchana wa siku ya Alhamisi Februari 1 baada ya bweni moja lenye vitanda zaidi ya 100 kuchomeka Jumatano usiku, wakati wanafunzi wa shule hiyo wakiwa darasani kwa masomo ya jioni.

Halmashauri ya shule hiyo pamoja na idara ya elimu katika eneo bunge la Kaloleni ilisema uamuzi huo wa kufungwa kwa shule hiyo ni kufuatia hasara iliyosababishwa na kuungua kwa bweni hilo ambapo bidhaa nyingi za wanafunzi zimechomeka.

Bwana Gerald Ngumbao, ni mwenyekiti wa halmashauri ya shule hiyo.

“Watoto wetu wote wapo salama hakuna aliyefariki kama inavyodaiwa katika mitandao ya kijamii, bweni likichomeka watoto walikuwa darasani wakisoma.

Na kama halmashauri ya shule tumewaruhusu wazazi kuwachukua watoto wao kwa siku hizi nne tunatarajia warudi Jumatatu ama Jumanne wiki ijayo huku tukijipanga kutafuta mikakati ya haraka wakirudi kuwe na mahali pa kukaa,” alisema.

Viongozi mbalimbali walizuru shule hiyo na kuahidi kusaidia kutoa fedha za ukarabati wa sehemu iliyoteketea.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana amezuru shule hiyo na kuahidi kutoa shilingi milioni moja kununua malazi na vitanda vilivyochomeka ili kurejesha hali ya kawaida shuleni humo.

“Kwa sababu ya hali hii na Uchumi ulivyo nimewasiliana na Mkurugenzi wa bodi ya kitaifa ya CDF ili nipate milioni moja ya dharura ili tusaidie hii shule wanunue magodoro na vitanda, tukingojea mhandisi wa public works aje akague atuelezee kuhusu marekebisho haya na kama haliwezi tutafute pesa tujenge bweni la kisasa.” Alisema

BY ERICKSON KADZEHA