HabariNews

Idadi ya Waliofariki katika Mlipuko wa Gesi, Embakasi Yaongezeka

Watu watatu wamethibitishwa kufariki kufuatia mlipuko uliokumba kiwanda kimoja cha kujaza gesi eneo la Embakasi jijini Nairobi, usiku wa Alhamisi.

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema wawili kati ya hao wamefariki walipokuwa wakipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi West.

Mwaura alisema kuwa watu wengine 222 waliojeruhiwa wamefikishwa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi, ambapo 21 wamepelekwa Hospitaili ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta na 160 katika hospitali kuu ya Mama Lucy.

Wengine 19 waliojeruhiwa wamepelekwa hospitali ya Mbagathi kwa matibabu, 14 wamepelekwa hospitali ya Modern Komarock na wengine 8 hospitali ya Nairobi West.

Inaarifiwa kuwa lori lililokuwa limejazwa mitungi ya gesi lililipuka na kusababisha moto mkubwa uliosambaa hasa baada ya mtungi wa gesi kuruka na kugonga bohari la kiwanda cha Oriental.

Afisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu jijini Nairobi, Antony Mushiri amebaini kuwa 27 wameruhusiwa Kwenda nyumbani.

“Majeruhi wamepelekwa hospitali mbalimbali Nairobi, na maafisa wa Red Cross wanashugulikia wenye majeraha madogo madogo na kuna wengie 27 waliruhusiwa kwenda nyumbani,” alisema.

Haya yanajiri huku Mtu mmoja akikamatwa na maafisa wa upelelezi wa Idara ya Upelelezi nchini DCI, kufuatia mkasa huo wa moto uliosababisha vifo vya watu watatu hadi kufikia sasa.

Mtu huyo aliyetiwa mbaroni leo anaripotiwa kuwa Mlinzi wa Kituo cha kujaza gesi cha Kampuni ya Dadols, eneo ambalo ndilo kitovu cha mlipuko huo.

BY MJOMBA RASHID