HabariNews

EPRA Yabaini Kituo cha Gesi kilicholipuka Embakasi, Kilihudumu Kinyume cha Sheria

Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli EPRA imefichua kuwa kituo cha kujazia gesi cha Embakasi jijini Nairobi ambako mlipuko ulitokea usiku wa Alhamisi, kilikuwa kikihudumu kinyume cha sheria.

Mamlaka hiyo imesema ilikataa maombi yote ya awali yaliyowasilishwa kwao ya kutaka idhini ya kujenga kituo cha kuhifadhi na kujaza gesi katika eneo la Mradi huko Embakasi kufuatia sababu kadhaa ikiwemo eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya watu.

Katika taarifa waliyoitoa EPRA imebaini kuwa walipokea maombi kadhaa kuanzia mnamo Machi 19 2023, tarehe 20 mwezi Juni na kisha Julai 31 mwaka huo.

Kwa mujibu wa EPRA waliyakataa maombi yote hayo kwa kuwa hayakuwa yamekidhi vigezo vilivyowekwa vya Mtambo wa kuhifadhi na kujaza gesi katika eneo hilo maarufu LPG.

Aidha Mamlaka hiyo imesema sababu kuu ya kukataa maombi hayo ni kutokana na kushindwa kwa miundo kukidhi masafa ya wa usalama yaliyoainishwa katika Ubora wa Viwango vya Kenya.

Fauka ya hayo EPRA iliarifu kuwa hatua za kiutawala zinachukuliwa kuhakikisha kuwa leseni za viwanda vilivyoratibiwa kuwa na viwango duni vya usalama wa juu unaohitajika zinafutiliwa mbali.

“Aidha, hatua za kufuatilia na kutekeleza zinachukuliwa ikiwemo kuharibu mitambo ya viwanda vinavyohudumu kinyume cha sheria kote nchini ili kukabiliana na ubadhirifu katika sekta hiyo,” ilisema EPRA.

Haya yanajiri huku idadi ya waliofariki kutokana na mkasa wa mlipuko huko Embakasi Nairobi ikifikia watu watatu kwa sasa na na wale waliojeruhiwa wakikaribia 300.

BY MJOMBA RASHID