HabariNewsSiasa

Chebukati Pia anayo Haki Kuwa Jaji Mkuu Nchini; Asema Mudavadi

Waziri mwenye Mamlaka makuu Musalia Mudavadi amemkashifu kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa madai kuwa rais Ruto anapania kumweka aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kuwa Jaji Mkuu.

Akiongea wakati wa ibada ya Jumapili huko kaunti ya Kakamega iliyohudhuriwa na rais William Ruto, Mudavadi amepuuzilia mbali mbali madai hayo akisema kuwa idara ya mahakama iko huru na ina haki ya kumuandika kazi yeyote aliyefuzu na kutimiza vigezo hitajika kuwa jaji mkuu nchini.

Mudavadi amesema kuwa mkenya yeyote aliye na vigezo vyote hitajika vya wadhfa huo anayo haki ya kugombea wadhfa wowote nchini Kenya akisisitiza kuwa haifai kwa Upinzani kuashiria ni nani anapaswa kuchaguliwa na tume ya Huduma za Mahakama JSC.

Mkuu huyo wa mawaziri aidha amebaini kuwa hata Chebukati anaweza kuwa Jaji Mkuu nchini iwapo atatimiza viwango na hitajika.

Kauli yake inajiri siku moja tu baada ya kinara wa Azimio Raila Odinga kudai kuwepo kwa mipango ya kumfanya Chebukati kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa kisha jina lake kuwasilishwa kuwa Jaji Mkuu kabla ya uchaguzi mkuu 2027.

Odinga alidai kuwa mipango hiyo ya rais Ruto ilidhihirika wakati wa mkutano wa Ikulu kati yake na Jaji Mkuu Martha Koome na kwamba katika mojawapo ya mpango mkubwa kati ya mipango yake Rais ni kujenga urafiki na idara ya mahakama ili kupitisha ajenda zake.

BY MJOMBA RASHID