HabariLifestyleNewsSiasa

Odinga asema yu Tayari Kuwania Mwenyekiti wa AU, ipi hatma yake Kisiasa za Kitaifa?

Kiongozi wa mrengo wa Upinzani nchini Raila Odinga ametangaza rasmi kuwa yu tayari kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika, AU.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi mnamo Alhamisi, Raila alibaini kuwa amefanya majadiliano na ushauri wa kina na wendani wake kabla ya kufikia uamuzi wa kuwania wadhfa huo.

Alisema iwapo uongozi wa Bara Afrika utahitajia huduma zake basi yu tayari kujitolea kulihudumikia bara hili ili kuhakikisha bara Afrika linapiga hatua kiuchumi, uwekezaji na maendeleo.

“Nimeshauriana na marafiki zangu kwa kina, Uongozi wa Afrika ukihitajia huduma zangu niko tayari kujitolea kwa hali na mali kulihudumikia bara hili kuhakikisha Afrika inaiamarika kiuchumi na maendeleo. Na leo naweka hadharani kuwa ni tayari kuwania wadhfa wa Mwenyekiti wa AU,” alisema.

Odinga alionyesha kutoridhishwa na hali ya Wananchi wa kiafrika Kwenda mabara mengine kutokana na hali ngumu ya kiuchumi licha ya bara hili kuwa na raslimali za kutosha.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alijipigia debe akisema kuwa kutokana na muda wake wa kuhudumu kama mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kwa maendeleo ya miundombinu kuanzia 2018 hadi 2023 ana uwezo wa kugombea nafasi hiyo akisema ana uelewa mzuri kuhusiana na jamii na Uchumi wa bara lote.

“Nishahudumu katika AU kiwango cha Balozi wa Miundomsingi barani, wadhfa huo ulinipa fursa nzuri ya kujua mengi kila nchi ya Afrika. Afrika ni bara tajiri zaidi hapa duniani ki masuala ya madini na raslimali kwa jumla, lakini ni kitendawili tata kuwa licha kuwa tajiri kiraslimali bara hili ni maskini zaidi ya mabara mengine, na hali hii tunapaswa kuibadili,” alisema Odinga.

Odinga alisema kuwa tayari amefanya mazungumzo na  na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ambaye alikuwepo kikao hicho kuwahamasisha viongozi wengine kote barani kuhusiana na swala hilo.

Obasanjo alisema ni muda mwafaka sasa kwa Mwenyekiti wa AU kutokea eneo la Afrika Mashariki ikizingatiwa kiti hicho kitakuwa wazi mwaka ujao.

“Chini yam waka kutakuwa na ubadilishaji wa uongozi wa AU. Iwapo Muungano huu utatekeleza lengo linalotakiwa kutekelezwa basi itahitaji mtu sahihi na kwa wakati sahihi, na huu ndio wakati tunapaswa kuifanya AU iwe inavyopaswa kuwa na hivyo AU inahitaji mtu sahihi mwenye tajriba na uzoefu anayeelewa hali tuliyo nayo. Na ikiwa eneo hili litaweka kiongozi sahihi basi tutasonga mbele,” alisema Obasanjo.

Mwenyekiti wa sasa wa AU Moussa Faki kutoka Chad anatarajiwa kukamilisha mihula yake miwili ya uongozi mwaka ujao.

BY MJOMBA RASHID