HabariMombasaNews

Hospitali za Kibinafsi zaapa Kuacha kutoa Huduma kwa Wagonjwa wenye NHIF

Hospitali za Kibinafsi nchini sasa zinatishia kuacha kutoa huduma za afya kwa Wanaotumia NHIF kusaka matibabu katika hospitali hizo.

Hii ni kufuatia serikali kuchelewa kusambaza malipo ya kutosha ya NHIF katika hospitali hizo.

Katika taarifa Muungano wa Hospitali za Kibinafsi nchini, KAPH umetoa notisi siku 7 kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kutoa fedha zote zinazodaiwa na hospitali wanachama wake.

Mwenyekiti wa Muungano huo Dkt. Eric Musau ameeleza kuwa iwapo NHIF haitatii na kutekeleza malipo hayo ndani ya muda huo basi hospitali za kibinafsi nchini zitasitisha kutoa huduma kwa wanaotumia NHIF katika hospitali hizo.

Ameeleza kuwa hospitali zinadai fedha nyingi na malipo waliyopewa awali yalikuwa finyu akidai kuwa hospitali zimelazimika kuchukua mikopo ya gharama kubwa, kukosa kulipa malipo ya wasambazaji huduma na bidhaa na hata kuwafuta kazi wafanyakazi wake ili kuendelea kutoa huduma kwa wenye NHIF.

Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa NHIF/SHA inapaswa kutoa fedha zote wanazodaiwa siku 60 baada ya kutoa huduma kulingana na makubaliano ya mkataba walioafikiana.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Januari mwaka huu Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alizionya hospitali za kibinafsi dhidi ya kutoa rekodi feki za wagonjwa akisema kuwa hospitali zinazozidisha malipo kwenye rekodi zake za NHIF zitakachukuliwa hatua za kisheria.

BY MJOMBA RASHID