HabariLifestyleMazingiraMombasaNews

Kilifi yadhibiti kwa asilimia 95 magonjwa yanayotakana na ukosefu wa usafi.

Ulimwengu ukiadhimisha siku ya kunawa mikono kaunti ya Kilifi inajivunia kudhibiti kwa asilimia 95 magonjwa yanayotokana na ukosefu wa usafi.

Hamasa ya mara kwa mara inayotolewa kwa wakazi kaunti ya Kilifi inadaiwa kukinga maambukizi ya magonjwa yanayotokana na usafi, juhudi hizo zikionekana kuzaa matunda zaidi katika eneo bunge la Rabai.

Kulingana na Catherine Munyoki msimamizi wa kitengo cha kuzuia magonjwa na kuboresha afya kaunti ya Kilifi asilimia 85 ya wakazi eneo bunge la Rabai wamefanikiwa kutengeneza sehemu za kunawa mikono katika maboma yao.

Amesistiza kuwa kudumisha kanuni za usafi ni hatua muhimu ya kukabiliana na kujikinga na magonjwa.

“Tunaweza kusema kwamba kunawa mikono kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha maisha na pia kusaidia maisha. Japo wengi wao wamehamasishwa kuhusu umuhimu wa usafi na sasa hivi tumefikia takriban asilimia 85 katika kupeana vile vituo vya kunawa mikono katika maboma. Na tunaendelea kuwahimiza ili wazifahamu vyema kanuni za usafi na kuzifuata kila wakati.” alisema Bi. Munyoki.

Munyoki, ameeleza kuwa kaunti ya Kilifi imefanikiwa kudhibiti asilimia 95 ya magonjwa yanayotakana na usafi, akiongeza kuwa kwa zaidi ya kipindi cha miaka miwili sasa kaunti hiyo haijaripoti kisa chochote cha ugonjwa wa kipindupindu.

“Tunaweza kusema tuko takriban asilimia 95 ya kudhibiti magonjwa haya yanayotakana na usafi kwasababu hakujakuwa na mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu kaunti yetu kwa kiindi cha miaka miwili iliyopita licha ya kuwa kumeripotiwa visa vya ugonjwa wa kipindupindu katika kaunti nyingine kama jirani yetu Mombasa. Hii ni kuonesha kuwa tumeweza kudhibiti magonjwa ambayo yanaweza kusababishwa na ukosefu wa usafi.” alisema Bi. Munyoki

Kwa upande wao wakazi eneo bunge la Rabai wamelalamika kupitia changamoto kufuata kanuni za usafi kikamilifu hasa kunawa mikono kutokana na uhaba wa maji ambao umekuwa ukishuhudiwa eneo hilo.

“Hapo kwa maji, hapo! Mnatuambia tuoshe mikono lakini tuna changamoto kubwa ya maji kwasababu huku kwetu kuna uhaba mkubwa wa maji.

“Hatudhani iwapo kampeni hii itafanikiwa kwa asilimia 100 kutokana na ukosefu wa maji hapa. Tunalazimika kutembea mwendo mrefu sana kutafuta maji wakati mwingine tunalazimika kufuata maji huko Kombeni.

“Mafunzo tumeyapata kwamba tunawe mikono mara kwa mara lakini je tutalifanikisha vipi hili ikiwa changamoto kubwa huku kwetu ni maji?” walisema wakazi.

Hayo yamejiri wakati wa hafla ya kuadhimisha siku ya kunawa mikono ulimwenguni iliyoandaliwa kijiji cha Mkapuni, eneo bunge la Rabai.

 

Erickson Kadzeha.