Serikali inalenga kutumia asilimia 40 ya wahandisi wa hapa nchini katika miradi mbalimbali mikuu ya Serikali ya Kitaifa na Kaunti.
Naibu rais Rigathi Gachagua aliyasema haya na kuhakikisha kuwa manunuzi yote ya serikali ya hadi shilingi bilioni 1 yatatengewa Wakenya.
Akiongea katika Kongamano la 30 la Wahandisi nchini na la 18 la Wahandisi wa Kimataifa mjini Mombasa, Naibu huyo wa rais alibaini kuwa atawasilisha mswada bungeni kuhakikisha kuwa wahandisi nchini wanapewa kipaombele katika miradi mbalimbali.
Alisema kuwa katika mswada huo serikali inalenga kuweka bayana kipengee cha asilimia 40 ya Wakenya kupewa kipaombele dhidi ya wahandisi wa kigeni, ili kuhakikisha kuwa Waajiri wanawalipa moja kwa moja na kwa wakati.
“Manunuzi yote hadi shillingi billion 1,asilimia 40 ya miradi hiyo itengewe wakenya,kwenye mswada nlioupendekeza hapo awali,asilimia 40 ya nafasi za kazi zikabidhiwe wananchi na fedha zao walipwe moja kwa moja,”alisema Gachagua.
Wakati uo huo Gachagua alieleza kuwa Serikali ya Kenya Kwanza itashirikiana na wataalamu mbalimbali katika miradi ya maendeleo ikiwemo ule wa ujenzi wa nyumba za makazi ya bei nafuu.
Akiupigia debe mradi huo Gachagua alithibitisha kuwa utawafaidi Wakenya wote kwa kubuni nafasi zaidi za ajira na kuimarisha viwango vya maisha nchini, huku akiwarai wahandisi hao kuunga mkono mpango huo.
“Mpango huo unawahusu kwa kiwango kikubwa na nawaomba muweze kushirikiana nasi kuutekeleza na kuwa ni mradi mkubwa na nafasi yenu ni muhimu kwenye jambo hili.Watu walidhania ni jambo geni lakini tunapania kuenua viwango vya maisha kwa kuwapa makaazi ya bei nafuu pamoja na kubuni nafasi zaidi za ajira”,aliongeza Naibu Rais.
Kwa upande wake Mkuu wa Bodi ya Wahandisi nchini EBK Erastus Mwongera ameitaka serikali kuwapa wahandisi nafasi ya kuhudumu katika nafasi kuu za uongozi akisema hatua hiyo itapiga jeki utekelezwaji wa mipango ya maendeleo nchini.
“Tunashukuru kwa kuteuliwa kwa baadhi ya wahandisi katika nafasi kuu serikali na matunda ya hayo ni dhahiri kwani suala hilo litahakikisha utendakazi mwema na utekelezwaji mwafaka wa sera za serikali ili kuleta maendeleo”,alikariri Mhandisi Erastus.