Bunge la Kaunti ya Kilifi linatarajiwa kujadili ripoti za uhasibu ya mwaka wa 2017-2018, 2018-2019 kuhusu utendakazi na utumizi wa fedha katika shirika la usambazaji maji mjini Malindi MAWASCO mwishoni mwa mwezi huu.
Mwenyekiti wa kamati ya uhasibu katika bunge la kaunti hiyo George Baya anasema ripoti waliyopokea kutoka kwa shirika hilo inaonyesha hasara kubwa inayopata shirika la MAWASCO inatokana na utumizi wa maji ambao haujanakiliwa.
Baya amedokeza kuwa hali hiyo inachangiwa pakubwa na utumizi wa maji kinyume cha sheria na mabomba ya maji kupasuka.
Baya ambaye pia ni mwakilishi wa wadi ya Watamu eneo bunge la Kilifi Kaskazini amebainisha kuwa katika ripoti hiyo kwa mwaka shirika hilo limekuwa likipoteza Shillingi Millioni sitini.
Hata hivyo ameongeza kuwa huenda kuna ubadhirifu wa fedha katika shirika hilo kwani hesabu zao haziwiani na shirika la maji eneo la Pwani.
Hatua hio inajiri baada ya kilio kikubwa cha uhaba wa maji kutoka kwa wakaazi kaunti hiyo kuongezeka katika siku za hivi karibuni.