Habari

Hatma ya walimu 27 waliosimamishwa kazi sasa iko mikononi mwa TSC…..

Hatma ya walimu 27 waliosimamishwa kazi kwa madai ya kuhusika na visa vya udanganyifu wakati wa mtihani wa kitaifa wa KCSE uliokamilika hapo jana sasa iko mikononi mwa tume ya huduma kwa walimu TSC.

Waziri wa elimu profesa George Magoha anasema majina ya walimu hao yamewasilishwa kwa TSC ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Baadhi ya walimu hao walikuwa wasimamizi wa mtihani huo wa KCSE ulioanza tarehe 25 ya mwezi machi.

Aidha watu wengine 37 wakiwemo wanafunzi 3 wa vyuo vikuu ni miongoni mwa waliokamatwa kwa kujaribu kufanikisha udanganyifu  katika mtihani huo wa KCSE, huku Magoha akisisitiza kwamba watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Hapo awali Magoha alitangaza kwamba watahiniwa wote wa KCSE na KCPE watapokea matokeo yao kufuatia agizo la rais Uhuru Kenyatta, akisema watakaowajibishwa kwa udanganyifu ni wasimamizi wa mitihani na wala si waliojaribu kushiriki udanganyifu huo.

Ni Watahiniwa takriban 752, 891 waliofanya mtihani wa KCSE huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa tarehe 10 ya mwezi mei.

By News Desk