Zaidi ya familia elfu 27 zimeathirika na janga la ukame katika maeneo ya Lungalunga na Kinango kaunti ya Kwale.
Eneo la Samburu ndilo lililoathirika zaidi na makali hayo, kwani zaidi ya familia elfu 10 zimeathiriwa kwa mujibu wa takwmu za shirika la msalaba mwekundu.
Afisaa wa shirika hilo katika kaunti ya Kwale Mohammed Mwaenzi amesema asilimia 90 ya vidimbwi vya maji vimekauka hali ambayo imesababisha wakaazi kuhangaika kutafuta maji.
Wafugaji pia wanaendelea kuhangaika kuwatafutia mifugo wao malisho na hata maji huku baadhi ya mifugo hiyo wakipoteza maisha.
Haya yanajiri huku waziri wa ugatuzi anayeondoka Eugene Wamalwa leo asubuhi amezindua rasmi mpango wa utoaji wa chakula cha msaada kwa kaunti zinazokabiliwa na ukame na njaa.
Katika uzinduzi huo Wamalwa amesema kwa sasa pia watapeleka chakula cha mifugo wa zile kaunti ambazo mifugo wao wameathirika kutokana na ukosefu wa malisho.
Aidha amewahakikishia wakenya kuwa ifikapo juma lijalo chakula hiki kitakuwa kimewafikia walengwa.
Wakati huo huo ametumia fursa hio kumshukuru rais Uhuru Kenyatta kwa kuendelea kumwamini kwa kumhamisha kutoka wizara ya ugatuzi na sehemu kame na kumpeleka kwenye wizara ya ulinzi akisema yuko tayari kwa majukumu yake mapya.
BY NEWS DESK.