HabariNews

WAVUVI WATOA MAKATAA YA WIKI MOJA KWA SERIKALI

Wavuvi zaidi ya 300 kaunti hii ya Kilifi wametoa makataa ya wiki moja
kwa serikali ya kaunti ya Kilifi kukomesha kuwahangaishwa kwao
wanapoendeleza shughuli zao la sivyo waandamane.

Wakiongozwa na Shallo Issa, msimamizi mkuu wa wahudumu wa mashua katika
bandari ya mjini Kilifi, anasema hatua hii inafuatia wavuvi kukamatwa
mara kwa mara na mashirika mbali mbali yanayohusika na uvuvi kwa madai
ya kutumia nyavu zisizoruhusiwa.

Issa ameitaja hatua ya kukamatwa kwa wavuvi kuwa ukiukaji wa makubaliano
yaliyofanyika kati ya wavuvi na serikali ya kaunti ya Kilifi, ambapo
wavuvi hao wanadai kuruhusiwa kuendeleza uvuvi huku wakiepukana na
utumizi wa nyavu zilizopigwa marufuku.

Aidha wamepongeza hatua ya bunge la kaunti ya Lamu, kuangazia swala la
wavuvi kubughudhiwa pamoja na wavuvi wa eneo hilo kuwezeshwa kwa
kununuliwa vifaa vinavyoruhusiwa na serikali ya kaunti ya Lamu kwa
ushirikiano na shirika la msalaba mwekundu.

BY ERICKSON KADZEHA