HabariNews

IGAD YASISITIZA UMUHIMU WA KUZINGATIA UCHUMI SAMAWATI KWA MAENDELEO YA TAIFA

Uchumi samawati (blue economy) una uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa kasi wa uchumi wa taifa la Kenya na nchi wanachama wa IGAD kwa ujumla iwapo utatiliwa maanani vilivyo.

Haya ni kwa mujibu wa Mwakilishi wa shirika la IGAD nchini Kenya Daktari Fatma Adan.  Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa Kongamano la siku 3 la kuelimishana na kubadilishana mawazo kuhusu uchumi samawati lililowaleta pamoja washikadau wa sekta mbalimbali barani Afrika.

Dkt. Fatma amesema kuwa uvumbuzi katika Pwani ya Kenya na katika sekta ya ubaharia akipigia mfano pwani ya Mombasa, unaweza kuwa msingi mkuu wa kuzalisha chakula, kawi na ukuaji wa sekta ya usafiri miongoni mwa sekta nyengine.

Hata hivyo ameweka wazi kuwa kupitia mradi wa Uchumi samawati uliopokea ufadhili kutoka kwa serikali ya Uswidi, wanachama wake wameweza kupiga hatua katika kuweka mikakati itakayoboresha sekta ya uvuvi, utalii, uchukuzi wa baharini na uchimbaji madini.

Kongamano hilo pia limehudhuriwa na mwenyekiti wa Uchumi Samawati nchini gavana wa Lamu Issa Timamy na gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir.

By Khadijah Binti Mzee