HabariNews

Walanguzi wa bangi yenye thamani ya Milioni 3.4 wafikishwa mahakamani

Wanawake wawili walionaswa na dawa za kulevya aina ya bangi huko Likoni
kaunti ya Mombasa wamefikishwa mahakamani hii leo kwa kosa la ulanguzi
wa mihadarati.

Washukiwa hao wawili Angelina Mwambingu na Joyce Wairima Mureithi na
wengine ambao hawakuwa mahakamani wameshtakiwa kwa kosa la ulanguzi na
kuhifadhi bangi yenye thamani ya shilingi Milioni 3,352,500.

Mbele ya Hakimu Mkuu Mkaazi wa mahakama ya Mombasa Rita Orari, washukiwa
hao wamekana mashtaka hayo na wametozwa dhamana ya kima cha shilingi
150,000 kila mmoja.

Kesi hiyo itasikizwa mwezi ujao.

Huku hayo yakijiri Mwanamke mmoja raia wa Kenya anazuiliwa nchini India
baada ya kukamatwa akisafirisha mihadarati aina ya Cocaine yenye thamani
ya takribani shilingi milioni 380.

Mwanamke huyo aliyewasili nchini humo kupitia Addis Ababa nchini
Ethiopia amenaswa na mihadarati hiyo ambayo alikuwa ameificha kwenye
chupa 3 za whisky.

Chupa hizo zilikuwa na vibandiko vya black label kabla ya mamlaka ya
forodha nchini humo kufanya uchunguzi zaidi.
Kwenye mahojiano na maafisa wa forodha mwanamke huyo amefichua kuwa begi
alilokuwa amebeba lilikabidhiwa kwake jijini Nairobi na alipaswa
kulikabidhi kwa mtu mwengine huko New Delhi.

BY EDITORIAL DESK