HabariNews

Kenya Kutoa Ufadhili wa Masomo kwa Wanafunzi 100 kutoka Comoros

Rais William Ruto ametangaza kuwa serikali ya Kenya itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 100 kutoka nchini Comoro wanaotaka kusomea hapa nchini.

Akiongea siku ya Alhamisi kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya uhuru nchini Comoro, rais Ruto amesema kuwa serikali yake imejitolea kuendeleza ushirikiano na uhusiano mwema baiana ya mataifa hayo mawili.

Aidha rais amesema kuwa wanafunzi wa Comoro walioko hapa nchini watakuwa wakilipa karo sawia na wanafunzi wa Kenya.

“Kwa heshima ya ndugu yangu rais wenu, serikali ya Kenya itawapatia scholarship 100 kwa watoto wa kutoka hapa Comoros. Na vile vile kwa sababu ya udugu na urafiki, na watu wa Comoros vijana wenu wanafunzi wote wanaosomea Kenya sasa watalipishwa kama vile wao ni wakenya na si wageni tena,” alisema Rais Ruto.

Wakati huo huo rais Ruto ameahidi kuondoa visa kwa raia wote wa Comoro walio na stakabadhi sahihi za kusafiri kuja hapa nchini.

Kwa upande wake rais wa Comoros Azali Assouman ameunga mkono hatua hiyo huku akiondoa visa kwa wakenya wanaosafiri Kwenda nchini humo.

Marais hao wawili aidha wametia saini makubaliano ya kibiashara na maendeleo.

BY EDITORIAL DESK