HabariNews

Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga pamoja na spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire watasalia kizuizini kwa siku mbili zaidi.

Hakimu Mkuu katika mahakama Kuu ya Mombasa Martha Mutuku ameagiza kuzuiliwa kwao katika kituo cha polisi cha port hadi siku ya jumatatu atakapotoa uamuzi kuhusu iwapo wataachiliwa kwa dhamana au la.

Wengine ambao Mahakama hiyo imeagiza kuzuiliwa ni msadizi wa Chonga, Victor Katana pamoja na Patrick Chiro ambaye ni mfanyakazi katika afisi ya seneta wa kaunti hiyo Stewart Madzayo.

Hata hivyo licha ya mawakili wa washtakiwa kuiomba mahakama kutoa uamuzi wao leo siku ya Ijumaa, mahakama hiyo imeshikilia kufanya hivyo wiki ijayo kutokana na muda waliochukua kuwasilisha hoja zao mbele ya mahakama hiyo.

Wanne hao walikamatwa Jumatano asubuhi baada ya kutawanywa na polisi waliokuwa wakishika doria katika eneo la Mtwapa kuzuia uwezekano wa maandamano kufanyika.

Wakati huo huo mahakama hiyo iliamuru watu 15 waliokamatwa eneo la Mtwapa siku ya Jumatano kufuatia maandamano ya upinzani kuachiliwa kwa dhamana ya shillingi laki moja na kima cha shillingi 10,000 kila mmoja na kesi hiyo itatajwa tarehe 4 Agosti mwaka huu.

BY EDITORIAL DESK