FoodHabariNews

Uhaba wa Vitunguu Wapelekea Ongezeko la Bei ya Bidhaa hiyo Sokoni

Huenda wananchi wakagharamika zaidi kununua bidhaa aina ya kitunguu kufuatia uhaba wa bidhaa hiyo nchini.

Meza yetu ya Biashara imebaini kuwa bidhaa hiyo imepanda maradufu ikilinganishwa na siku za hivi karibuni.

Wafanyabiashara wa bidhaa hiyo katika soko la Marikiti jijini Mombasa wameeleza kuwa mvua nyingi ilioshuhudiwa kwa takriban mwezi mmoja sasa imechangia changamoto hiyo ya uhaba wa bidhaa hiyo kwa kuharibu zao hilo shambani.

David Gitau mmoja wa Wafanyabiashara hao amesema kuwa idadi ndogo iliyosalia inauzwa kwa bei ghali pamoja na kutoa bidhaa hiyo kutoka mataifa ya nje hivyo basi kuwalazimu kuwauzia wateja wao kwa bei ya juu.

“Kule mashambani kulinyesha zaidi kukaharibiwa na mvua, kisha wale wakulima safari hii hawakulima kitunguu sana,wengi walipanda mahindi.” Alisema Gitau.

Kwa sasa kilo ya vitunguu inauzwa kwa shillingi 200 ambapo awali ilikuwa ikiuzwa kwa shilling 80 na neti ikiuzwa kwa shillingi 2,000 ambapo ilikuwa ikiuzwa kwa shillingi 700, huku kitunguu saumu ikiuzwa kwa shilling 600 kwa kilo ambapo ilikuwa ikiuzwa kwa shilling 400 na 30 kwa bei ya rejareja ambapo ilikuwa ikiuzwa kwa shilling 10.

“Hapa kitunguu inayokuja inatoka Tanzania na Ethiopia ndio maana bei yake imeenda juu.” Alisema mfanyabiashra mwengine.

Wauzaji hao aidha wamelalamikia kudorora kwa biashara ya bidhaa hiyo wakisema wateja wananunua kiwango kidogo kinyume na hapo awali na wamewataka serikali kuingilia kati kuwanusuru kilimo cha bidhaa hiyo kutokana na utumizi wake mkubwa humu nchini.

“Wateja wanalalamika maanake hiyo bei ni ya juu,tulikuwa tunauza shilling 50 sasa imepanda zaidi,wanakuja lakini hawanunui kama pale mbeleni, mtu yule alikuwa akichukua kilo anachukua nusu na nusu anachukua robo.”alikariri mfanyabiashara

Kwa upande wao wateja wamesema kuwa imewabidi kununua idadi ndogo na kutumia kiwango kidogo kufuatia gharama ya juu ya maisha.

BY EDITORIAL DESK