HabariNews

Serikali za kaunti Pwani zalaumiwa kwa kukosa kuwajibikia mizozo ya ardhi eneo hili

Viongozi wa kijamii wanadai kuwepo ulegevu katika serikali za kaunti hasa kwenye suala la kuwatetea wakazi wake wasinyang’anywe ardhi zao na mabwenyenye hali inayodaiwa kuzidi kuacha familia nyingi kuwa maskwota.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama cha Mijikenda-Taireni Peter Ponda, anasema serikali za kaunti zimekuwa na ulegevu wa kukabiliana na changamoto hiyo kufuatia kukosa kuhudhuria vikao vinavyohusu mizozo hiyo ya ardhi mahakamani.

“Masikitiko yetu ni kuwa Kwale, Kilifi na kule Lamu, hakuna siku moja Serikali ya kaunti imekuja Koritini kuongelea kesi zetu za ardhi ambazo sasa zinaenda kumalizika na tumekuwa tukiwaalika. Inaonesha wazi wanaogopa kwa kuwa wanajihusisha na mabwenyenye hao wanaochukua ardhi za wananchi.” Akaongezea Bw. Ponda

Ameeleza kuwa licha ya mashirika ya kijamii kuweka juhudi ya kufuatilia kesi hizo mahakamani, serikali za kaunti hazijaonyesha ari ya ushirikiano na mashirika hayo katika kutatua mizozo hiyo.

Kwa upande wake spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire, amesema serikali za kaunti hazifai kulaumiwa kutokana na kesi nyingi za mizozo ya ardhi.

Akiongea katika kikao na mwanahabari wetu Mwambire zinashughulikiwa na serikali ya kitaifa.

Ametoa wito kwa mashirika ya kijamii kushirikiana katika kutafuta suluhu ya mizozo hiyo badala ya kunyosheana kidole cha lawama.

Ikumbukwe kuwa maeneo mengi Ukanda wa Pwani yamekuwa yakishuhudia mizozo ya ardhi ambayo imewaacha wakazi wengi maskwota wa makaazi yao ya muda mrefu.

BY EDITORIAL DESK