HabariNews

Fahamu Wabunge Bubu Waliofyata ulimi Bungeni Kwa Mwaka mmoja

Huku ikiwa ni mwaka mmoja tangu Wakenya walipotekeleza demokrasia ya kuwachagua viongozi katika nyadhfa mbalimbali, wakiwemo wabunge utafiti unabainisha wakenya wangali wanasubiria kuwakilishwa vilivyo bungeni.

Ripoti ya Shrika la Mzalendo Trust imefichua kuwa zaidi ya wabunge 15 hawajawahi kuchangia suala lolote kwa muda wa zaidi ya miezi 10 tangu kuchaguliwa kuwakilisha bungeni.

Ripoti hiyo iliyoangazia shughuli na matokeo ya uchangiaji hoja wakati wa mijadala muhimu bungeni katika kipindi hicho aidha imebaini kuwa kuna wabunge ambao hawajafungua kinywa tangu kuapishwa kwao katika bunge la Kitaifa.

Wabunge hao ni pamoja na Feisal Bader wa Msambweni, Mbunge wa Mvita Mohamed Soud Machele, Mbunge wa Mlima ELgon Fred Kapondi, Innocent Momanyi wa eneobunge la Bobasi, Ernest Ogesi wa Vihiga, Mbunge Mteule Joseph Iraya Wainaina na Elizabeth Kailemia, Meru.

Wengine ambao wangali kufungua kinywa chao kuchangia hoja na mijadala bungeni ni Mwakilishi wa Kike kaunti ya Lamu Muthoni Marubu, Mwakilishi wa Kike wa Meru Elizabeth Kailemia, Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri, Paul Chebor wa Rongai, Ernest Kagesi wa Vihiga.

Aidha ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano Agosti 9 imefichua kuwepo kwa wabunge wa bunge lililopita la 12 ambao wameendelea kusalia kimya bungeni wakikosa kuchangia mijadala muhimu kwa muda huo.

Baadhi ya Wabunge hao ni pamoja na Oscar Sudi ambaye ni mbunge wa Kapsaret, Mbunge wa Makadara George Aladwa na Samuel Arama wa Nakuru miongoni mwa wengine.

Ripoti hiyo aidha imeangazia wabunge waliokuwa mstari wa mbele kuchangia mijadala ambao ni pamoja na Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, Beatrice Elachi wa Dagoretti Kaskazini, David Makali wa Kitui ya Kati miongoni mwa wengine.

NA MJOMBA RASHID